Upinzani waamini utashinda uchaguzi Myanmar

Myanmar Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Chama cha NLD kina matumaini ya kushinda asilimia 70 ya viti vya ubunge

Chama cha upinzani nchini Myanmar National League for Democracy kimesema kina Imani kitashinda uchaguzi wa kwanza huru kufanyika nchini humo katika kipindi cha miaka 25.

Msemaji wa NLD amesema chama hicho kinatarajia kushinda asilimia 70 ya viti vyote vya ubunge nchini humo.

Kiongozi wa chama hicho Aung San Suu Kyi amesema: "Nadhani nyote mnaweza kukisia matokeo yatakuwa vipi.”

Matokeo ya kwanza rasmi yametolewa kutoka maeneo bunge 12, na viti hivyo vyote vimetwaliwa na NLD.

Chama cha Union Solidarity Development Party (USDP) kinachoungwa mkono na jeshi kimekuwa madarakani tangu 2011.

“Tunaelekea kushinda asilimia 70 ya viti kote nchini, lakini tume ya uchaguzi bado haijathibitisha hili,” msemaji wa NLD Win Htein aliambia shirika la habari la AFP.

Kaimu mwenyekiti wa chama cha USDP ameambia BBC Burmese kwamba amepoteza kiti chake cha ubunge katika eneo la Hinthada, jambo ambalo linachukuliwa kama ishara kubwa kuhusu mwelekeo wa matokeo.

"Tutatafuta kujua ni kwa nini tumeshindwa," U Htay Oo amesema. “Hata hivyo, tunakubali matokeo bla masharti yoyote. Bado hatujajua matokeo kamili ya mwisho yatakuwaje.”

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bi Suu Kyi, ambaye haruhusiwi kuwania urais, amesema chaka chake kikishinda atakuwa "juu ya rais"

Awali, Bi Suu Kyi aliwahutubia wananchi makao makuu ya NLD mjini Yangon, na kuwaomba wawe na subira.

Robo ya viti vya bunge nchini humo vimetengewa jeshi, na ili NLD ipate wingi wa viti, lazima ishinde angalau thuluthi mbili ya viti vilivyosalia.

Bi Suu Kyi hawezi kuwa rais kwani katiba ya nchi hiyo inamzuia mtu mwenye watoto ambao ni raia wa kigeni kuongoza. Wanawe wawili wa kiume, pamoja na mumewe marehemu, ni raia wa Uingereza.

Iwapo chama hicho kitashinda, huenda kikapendekeza mtu mwingine kuwa rais. Bi Suu Kyi hata hivyo tayari amesema atakuwa “juu ya rais.”