Kiongozi wa zamani wa Ujerumani afariki

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Schmidt alipigana Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

Helmut Schmidt, aliyehudumu kama Chansela wa Ujerumani Magharibi kuanzia 1974 hadi 1982 amefariki akiwa na umri wa miaka 96.

Bw Schmidt, aliyekuwa wa chama cha Social Democrat, alihusika kuunda mfumo wa kuunganisha sarafu za Ulaya ambao mwishowe ulipelekea kuanzishwa kwa sarafu ya euro. Kadhalika, alisaidia kuendeleza ufanisi wa kiuchumi wa Ujerumani baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Chansela Angela Merkel alimtaja kama mtu aliyekuwa "taasi ya kisiasaā€¯ nchini Ujerumani.

Yeye hutazamwa kama mmoja wa viongozi washuhuri zaidi Ujerumani tangu kumalizika kwa vita hivyo.

Bw Schmidt alifariki Jumanne adhuhuri akiwa nyumbani mwake katika jiji la Hamburg, daktari wake Heiner Greten alinukuliwa na vyombo vya habari Ujerumani, ingawa hakusema kilichosababisha kifo chake.

Kabla ya kuwa kiongozi Bw Schmidt alihudumu kama waziri wa fedha katika serikali ya Willy Brandt.

Wakati wa vita baridi, alichangia sana katika kukabili ubabe wa viongozi wa Muungano wa Usovieti Ulaya.

Bw Schmidt alizaliwa Hamburg 1918, mwezi mmoja baada ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Schmidt alitekwa na majeshi ya Uingereza 1944

Akiwa na umri wa miaka 14, viongozi wa Nazi walipochukua mamlaka, alikuwa kiongozi katika kundi la Vijana wa Hitler na alijiunga na jeshi la Ujerumani 1937. Alipigana Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kupanda cheo hadi kuwa luteni. Alitekwa na Waingereza Vita vya Bulge wakati wa majira ya baridi 1944-45.

Akiwa mateka, alishawishiwa na wafungwa wenzake kujiunga na siasa za Social Democrat. Alifuzu kutoka Chuo KIkuu cha Hamburg 1949, ambako alikuwa mwenyekiti wa chama cha wanafunzi wa Social Democrats. Baadaye, alijiunga na serikali na kuwa mshauri wa kiuchumi wa serikali ya Hamburg.

Alichaguliwa katika bunge la jimbo 1953 ambapo uwezo wake wa kuhutubu ulimfanya kupewa jina la utani "Schmidt-Schnauze" (Schmidt mwenye mdomo mkubwa).