Polisi wanane wafungwa jela Afrika Kusini

Haki miliki ya picha
Image caption Mauaji ya Macia yalisababisha maandamano mjini Johannesburg

Maafisa wanane wa polisi waliopatikana na hatia ya kumtendea unyama dereva wa teksi kutoka Msumbiji mwaka 2013 wamehukumiwa kifungo cha miaka 15 kila mmoja.

Jaji Bert Bam amesema kitendo walichofanya maafisa hao wa polisi ni cha kinyama.

Baada ya kuwaagiza wasimame kizimbani, amewaambia "kila mmoja wenu anahukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.”

Jaji huyo amesema mauaji hayo hayakukusudiwa.

Maafisa hao walinaswa kwenye kanda ya video wakimbrurura dereva wa teksi kutoka Msumbuji aliyetambuliwa kama Macia mwenye umri wa miaka 27 mtaa wa Macia mashariki mwa Johannesburg. Macia alikuwa amesimamishwa na maafisa tisa wa polisi kwa kosa la kuvunja sheria za trafiki, lakini baadaye kukatokea mfarakano.

Mmoja wa maafisa hao hakupatikana na hatia.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Macia alifungiwa nyuma ya gari na kubururwa karibu mita 200

Video ya kisa hicho ilisambaa sana katika mitandao ya kijamii.

Ukumbi wa mahakama mjini Johannesburg ulikuwa umejaa jamaa za maafisa hao wa polisi pamoja na wanahabari.

Raia waliozungumza na BBC wanasema hukumu hiyo itakuwa funzo kwa maafisa wa polisi dhidi ya kutumia vibaya mamlaka yao wakiwa kazini.