Tunayojua kwa sasa kuhusu mashambulio Paris

Hollande Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Hollande ameapa kukabiliana na waliohusika "bila huruma"

Wavamizi wameshambulia maeneo sita mjini Paris na kuua zaidi ya watu 120. Haya hapo ni maelezo muhimu kuhusu mashambulio hayo ambayo tunatajua kufikia sasa:

Waathiriwa

Watu 120 wamefariki, 200 wamejeruhiwa, 80 wakiwa hali mahututi

Maeneo yaliyoshambuliwa

  • Baa ya Le Carillon, barabara ya 18 rue Alibert, mtaa nambari 10 – ulishambuliwa kwa bunduki
  • Mghahawa wa Le Petit Cambodge, barabara ya 20 rue Alibert, mtaa nambari 10-, ulishambuliwa kwa bunduki
  • Uwanja wa Stade de France, St Denis, kaskazini mwa Paris – mlipuko ulitokea nje ya uwanja huo wakati wa mechi ya kirafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani
  • La Belle Equipe, barabara ya 92 rue de Charonne, mtaa nambari 11 – ulishambuliwa kwa bunduki
  • Ukumbi wa sanaa wa Bataclan, barabara ya 50 boulevard Voltaire, mtaa nambari 11 – ulishambuliwa kwa bunduki, na watu kushindwa mateka
  • Mghahawa wa La Casa Nostra, barabara ya rue de la Fontaine au roi, mtaa nambari 11 - ulishambuliwa kwa bunduki
Haki miliki ya picha AP
Image caption Watu 200 wamejeruhiwa

Mashambulio yalitokea saa ngapi?

Mashambulio yalitekelezwa mwendo wa saa nne saa za Ufaransa, watu wengi walikuwa kwenye maeneo hayo ya burudani ikizingatiwa kwamba ilikuwa usiku wa ijumaa.

Washambuliaji wako wapi?

Washambuliaji wanane wamefariki, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP. Saba walijilipua, na mmoja akauawa. Wanne walifariki katika ukumbi wa Bataclan, watatu kwa kujilipua na mmoja akauawa na polisi.

Watatu walifariki karibu na uwanja wa michezo wa taifa naye wa nne akauawa barabarani mashariki mwa Paris.

Rais Francois Hollande anafanya nini?

Rais alihutubia taifa kupitia runinga, akatangaza hali ya hatari na kufunga mipaka ya taifa na baadaye akazuru ukumbi wa Bataclan ambako watu karibu 100 waliuawa. Ameahidi kukabiliana na waliohusika “bila huruma”.

Aidha, ameahirisha ziara aliyokuwa amepanga kuifanya kwenda Uturuki kwa mkutano wa G20.

Nani walihusika?

Kufikia sasa hakuna aliyedai kuhusika katika mashambulio hayo. Aidha, haijabainika sababu yao kushambulia lakini mmoja wa walioshuhudia shambulio Bataclan amesema alimsikia mmoja wa wavamizi akieleza uungaji mkono wake kwa wapiganaji wa Islamic State.

"Hollande ndiye aliyesababisha haya, hangeingilia mzozo Syria!" mshambuliaji huyo alisema, kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa AFP.

Washambuliaji walitumia nini?

Walioshuhudia wanasema washambuliaji walitumia bunduki aina ya AK na walikuwa wamejifunga mikanda ya kujilipua. Baadhi ya maeneo yalilipuliwa kwa mabomu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Obama ameahidi kusaidia kukabiliana na magaidi

Viongozi wanasema nini?

Rais wa Marekani Barack Obama amesema: "Hili si shambulio tu dhidi ya raia wa Ufaransa. Ni shambulio dhidi ya binadamu wote na maadili yetu ya pamoja. Tutafanya kila tuwezalo kuwasaidia watu wa Ufaransa na mataifa kote duniani kuhakikisha magaidi hawa wanakabiliwa.”

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron naye ameshutumu shambulio hilo na kuahidi usaidizi kwa Ufaransa.

Rais wa Uchina Xi Jinping naye pia ameshutumu shambulio hilo, akatuma risala za rambirambi na kuahidi kushirikiana kukabiliana na magaidi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameshutumu mashambulio yaliyotekelezwa mjini Paris. Msemaji wa UN Stephane Dujarric amesema Ban ''anaamini Ufaransa ina uwezo wa kuwakamata na kuwatendea haki wahusika upesi."

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ameshtushwa sana na “habari na picha zinazotufikia kutoka Paris”. Amesema anaomboleza na waathiriwa wa “linalodhihirika kuwa shambulio la kigaidi”.

Waziri mkuu mpya wa Canada Justin Trudeau amesema wako pamoja na “binamu zetu Wafaransa wakati huu wa giza na majonzi”. Ameahidi kuisaidia serikali ya Ufaransa.