US yasema ina uhakika kiasi Jihadi John aliuawa

Jihadi John
Image caption Jihadi John alikuwa akionekana kwenye video zilizoonyesha mateka wakiuawa kwa kukatwa shingo

Marekani imesema ina uhakika fulani kwamba mwanamgambo wa Islamic State anayejulikana sana kama Jihadi John, aliyelengwa kwenye shambulio Syria Alhamisi, aliuawa.

Kanali Steve Warren wa Pentagon alisema shambulio hilo la Alhamisi mjini Raqqa lilipata shabaha, lakini itachukua muda “kutangaza rasmi kwamba shambulio hilo lilifanikiwa”.

Mohammed Emwazi, raia wa Uingereza aliyezaliwa Kuwaiti, alionekana kwenye video akikata shingo mateka kutoka mataifa ya Magharibi.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alisema kumlenga Emwazi lilikuwa “jambo sahihi”.

Inaaminika kwamba kuna mtu mwingine mmoja kwenye gari lililolengwa ambalo lilikuwa limembeba Emwazi, anayejulikana sana kama Jihadi John.

Kanali Warren alisema mashambulio ya mara kwa mara ya Marekani yamekuwa yakiua karibu “kiongoni mmoja mkuu au wa ngazi ya kati wa IS kila siku mbili” tangu mwezi Mei.

Hata hivyo, kifo cha Emwazi kitakuwa “pigo kuu” kwa IS, ingawa hajakuwa akihusika sana katika mipango ya IS au katika uongozi wa kundi hilo.

Kwingineko, maafisa nchini Uturuki wanasema wamemkamata mwanamume raia wa Uingereza, anayeaminika kuwa Aine Lesley Davis, anayedaiwa kuwa mshirika wa Jihadi John. Aine Davis anadaiwa kuwa mmoja wa waliokuwa wakilinda mateka kutoka mataifa ya Magharibi nchini Syria.