Paris: Vyombo vya habari vilibagua Garissa?

Image caption 'Occupy Wall St' ndio waliotibua mjadala huo

Licha ya BBC na mashirika mengine ya habari kupeperusha habari kuhusu shambulizi la Paris Ufaransa usiku wa Ijumaa hadi leo, katika mitandao habari inayogonga vichwa vya habari ni ile ya shambulizi la kundi la wanamgambo wa Alshabaab nchini Kenya lililosababisha vifo vya wanafunzi 147.

Ripoti hii ambayo ilitamausha ulimwengu yapata miezi 6 iliyopita ndio inayosambazwa zaidi.

Aidha ripoti hii kuhusu shambulizi ambapo wapiganaji wa kundi la Al shabaab walivamia wanafunzi na kuwapiga risasi ndiyo iliyosomwa zaidi, huku kukiibuka mjadala kuhusu kuangaziwa kwa shambulio la Paris.

Wasomaji wengi wanaikashifu muda zaidi uliopewa ripoti kuhusu shambulizi la Paris ambapo watu 129 walipoteza maisha yao ikilinganishwa na muda uliopewa ripoti kuhusu shambulio hilo sawa kaskazini mashariki mwa Kenya.

Image caption Waliouawa katika chuo kikuu cha Garissa

Shambulio hilo katika Chuo Kikuu cha Garissa lilisababisha wanafunzi 147 kupoteza maisha yao.

Hii inafuatia hatua ya kundi la 'Occupy Wall St' kuichapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Facebook swali likiuliza, Je mnakumbuka kuwa huko nchini kenya wanafunzi 147 walipoteza maisha yao?

Kisha, tovuti hiyo iliweka kiunganishi cha habari kuhusu shambulio hilo la Garissa na kuwafanya watu kuisoma sana.

Image caption Wanafunzi 147 walipoteza maisha yao mwezi Aprili

Kundi hilo linashangaa ni kwanini idhaa zote za dunia hazikulipa tukio hilo kipaombele kama wanavyolipa shambulio la Paris ilhali wanafunzi wengi zaidi 147 walipoteza maisha yao al-Shabab ilipovamia chuo kikuu hicho mapema mwezi Aprili.

Ripoti hiyo ambayo mwishowe ilifika kwenye Reddit na kuenea sana iliwaacha watu wengi wamepigwa na butwaa huku wengine wakifoka kwa hasira na kudai kuwa 'Occupy Wall St' inajaribu kuashiria kuwepo kwa ubaguzi.