Mkuu wa UN kuzuru Korea Kaskazini

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ni makatibu wawili pekee wa UN waliowahi kuzuru Korea Kaskazini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon atazuru Korea Kaskazini wiki hii, kwa mujibu wa shirika la habari la Korea Kusini Yonhap.

Yonhap wamenukuu afisa wa ngazi ya juu wa UN, ingawa umoja huo umekataa kuzungumzia habari hizo.

Ziara hiyo ikifanyika basi itakuwa mara ya kwanza kwa mkuu wa UN kuzuru taifa hilo katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili.

Mwezi Mei, Korea Kaskazini ilifutilia mbali ziara ya Bw Ban siku moja tu kabla yake kuwasili.

Korea Kaskazini imewekwa vikwazo na UN , EU na Marekani kutokana na hatua yake ya kufanya majaribio ya nyuklia.

Habari hizo za shirika la Yonhap zimesema kuna uwezekano mkubwa kwamba atakutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un wakati wa ziara hiyo.

Tarehe kamili ya ziara hiyo haikutolewa.

Bw Ban, ambaye ni waziri wa zamani wa mashauri ya kigeni wa Korea Kusini, atakuwa katibu mkuu wa tatu wa umoja huo kuzuru Korea Kaskazini.

Umoja wa Mataifa uliunga mkono Korea Kusini wakati wa Vita vya Korea, vilivyodumu kuanzia 1950 hadi 1953 na kupelekea kugawanyika kwa Korea.