11 wauawa kambi ya Wakimbizi,Somalia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wakimbizi wa Somalia

Idara za Usalama katika kambi ya wakimbizi mjini Mogadishu zimeeleza kuwa watu 11 wameuawa kutokana na mapigano yaliyozuka wakati wakiwa katika mstari kupokea chakula cha msaada.

Meya wa mji wa Mogadishu Yusuf Hussein Jimale amesema kuwa katika tukio hilo kati ya waliouawa wengi wao ni wanawake na watoto.

Amesema kuwa tayari watuhumiwa katika mauaji hayo wanashikiliwa na vyombo vya Usalama.Amesema mtu aliyejifanya ni mlinzi wa eneo hilo ambaye anatoka katika makundi ya kigaidi alianza kuwashambulia watu waliopo eneo hilo huku akihitaji kujua ni wapi alikuwa kiongozi wa utoaji msaada huo.

Hata hivyo vikosi vya usalama vilianza kurushiana risasi na washambuliaji hao waliokuwa wamejichanganya na watu na kisha kusababisha mauaji hayo.

Nyumba za watu katika kambi hiyo ni za wale waliyoyakimbia makazi yao kutokana na kundi la Al Shabab na ukame wa muda mrefu na mzozo nchini Somalia.