Mauaji ya Paris yalipangwa nchini Syria

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mauaji ya Paris yalipangwa nchini Syria

Waziri mkuu wa Ufaransa, Manuel Valls, amesema polisi wamegundua kuwa mauaji yaliyotokea mjini Paris Ufaransa siku ya Ijumaa yalipangwa nchini Syria.

Aidha Valls ameonya kuwa mashambulizi zaidi yanapangwa dhidi ya Ufaransa na mataifa mengine ya bara Ulaya.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Waziri mkuu huyo anasena kuwa polisi wamekuwa wakiendesha msako mkali katika maeneo yote wanayoyashuku nchini

Waziri mkuu huyo anasena kuwa polisi wamekuwa wakiendesha msako mkali katika maeneo yote wanayoyashuku nchini humo huku uchunguzi ukiendelea kuhusu mashambulio ya kigaidi ya ijumaa usiku.

Mojawapo ya maeneo yaliyovamiwa ni Bobigny, Kazkazini Mashariki mwa Paris, maeneo ya Toulouse karibu na mpaka na Ubelgiji.

Watu kadhaa wamekamatwa na wanahojiwa.

Hayo yanajiri huku ikibainika kwamba mtuhumiwa mkuu wa mashambulio hayo ya Paris ambaye kwa sasa anasakwa, aliwahi kusimamishwa na polisi na kuachiliwa saa chache tu kabla ya mashambulio hayo kufanyika.

Maafisa polisi walisimamisha gari la Salah Abdeslam, mwenye umri wa miaka 26 alipokuwa akielekea mpakani mwa nchi hiyo na Ubelgiji.

Nduguye wawili ambao wanasemekana ni miongoni mwa washambuliaji, mmoja aliuawa wakati wa tukio na mwengine kukamatwa.

Wakati huohuo, ndege za kivita za Ufaransa zimefanya mashambulio ya kulipiza kisasi huko Syria mjini Raqqa, dhidi ya wanamgambo wa IS.

Harakati hizo za mashambulio zimeongezwa siku mbili tu baada ya kundi hilo kujitaja kwamba ndilo lililohusika na mashambulio ya risasi na kujitoa muhanga yaliyoukumba mji mkuu wa Ufaransa Paris yaliyowauwa zaidi ya watu 129.

IS wamesema walifanya mashambulio hayo baada ya Ufaransa kujiunga na vikosi vya muungano ambao umekuwa ukishambulia kundi hilo.

Wizara ya ulinzi ya Ufaransa imesema Operesheni zao huko Syria zimelenga mahandaki ya kundi hilo, na maeneo yanayotumiwa na kundi hilo kwa mafunzo na mazoezi .

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ndege za kivita za Ufaransa zimefanya mashambulio ya kulipiza kisasi huko Syria mjini Raqqa, dhidi ya wanamgambo wa IS.

Ndege 12 zimeshiriki Operesheni hiyo zikidondosha mabomu 20.

Baadaye leo rais wa Ufaransa Francois Hollande, ataongoza taifa hilo katika muda wa kukaa kimya kuwakumbuka watu hao 129 waliofariki katika mashambulizi ya kigaidi.

Bw. Hollande atalihutubia Bunge la taifa hilo.

Baadhi ya maeneo yanayopenda kutembelewa na umma yaliyokuwa yamefungwa sasa yatafunguliwa tena