Urusi yashambulia Islamic State

Image caption Shambulizi la roketi dhidi ya Islamic State

Urusi imesema kuwa imetekeleza shambulio kali zaidi dhidi ya maeneo yanayokaliwa na wapiganaji wa Islamic State nchini Syria,ikiwa ni miongoni mwa mashambulizi yake ya hewani kufikia sasa.

Waziri wa ulinzi Sergei Shoigu,amethibitisha ripoti za Ufaransa na Marekani kwamba Moscow ilitumia mabomu ya masafa marefu na makombora .

Amesema kuwa ndege hiyo ilirusha makombora katika maeneo ya wapiganaji hao mjini Raqqa,ambao ndio ngome kuu ya wapiganaji hao na Deir ez Zor mashariki mwa Syria,huku mabomu yakilenga Kaskazini.

Awali rais Vladmir Putin alionya mashambulizi makali dhidi ya IS,kufuatia thibitisho kwamba ndege ya Urusi ilioanguka nchini Misri mwezi uliopita ilisababishwa na shambulizi la kigaidi.

Maafisa wa Urusi wanasema kuwa chembechembe za vilipuzi zilionekana katika mabaki ya ndege hiyo aina Airbus.

Abiria wote 224 walioabiri ndege hiyo ,wengi wao wakiwa watalii wa Urusi waliuawa.

Kundi la Islamic State limethibitisha kutekeleza shambulio hilo.