Wawili wauawa msako wa mshukiwa Paris

Haki miliki ya picha AP
Image caption Maafisa walizingira sehemu ya mtaa wa Saint Denis wakisaka washukiwa wa mashambulio ya Ijumaa

Mwanamke amejilipua na mshukiwa mmoja akauawa kwa kupigwa risasi wakati wa operesheni ya polisi katika mtaa mmoja wa Paris.

Watu saba wamekamatwa.

Polisi walishambulia nyumba moja mtaa wa Saint Denis wakisama mshukiwa anayedaiwa kupanga mashambulio ya kigaidi ya Ijumaa ambayo yalisababisha vifo vya watu 129 mjini Paris.

Hatima ya mshukiwa huyo,Abdelhamid Abaaoud, ambaye awali alidhaniwa kuwa nchini Syria bado haijulikani.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Hatima ya mshukiwa mkuu Abdel Abaaoud aliyekuwa akisakwa haijabainika

Mkuu wa mashtaka Francois Molins alisema habari za kijasusi zilikuwa zimedokeza kwamba yumo mjini Paris.

Wote waliofariki kwenye mashambulio hayo ya Ijumaa wametambuliwa, serikali imesema.

Kundi la Islamic State (IS) lilisema lilihusika kwenye mashambulio hayo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Maafisa watano wa polisi walijeruhiwa

Operesheni hiyo mtaani Saint-Denis, ambako uwanja wa taifa wa Stade de France unapatikana, ilianza mwendo wa saa kumi na dakika ishirini saa za Ufaransa.

Akiongea na wanahabari eneo la operesheni baadaye, Bw Molins alisema operesheni hiyo ilianzishwa baada ya udukuzi wa simu na habari za kijasusi kudokeza kuwa Abaaoud, Mbelgiji mwenye asili ya Morocco, huenda alikuwa nyumbani humo.

Mwanamashtaka huyo alisema mwanamke mmoja, ambaye kituo cha runinga cha BFMTV cha Ufaransa kilisema alikuwa jamaa wa Abaaoud, alijipua baada ya operesheni kuanza.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Polisi waliwaondoa raia kutoka eneo hilo wakati wa operesheni yao

Mshukiwa mwingine aliuawa na guruneti na risasi za polisi, Bw Molins alisema.

Maafisa watano wa polisi wa kikosi maalum cha kupambana na ugaidi cha RAID waliohusika kwenye operesheni hiyo walipata majeraha madogo.

Mbwa wa kikosi hicho cha polisi kwa jina Diesel mwenye umri wa miaka saba pia aliuawa.

Wanaume watatu walikamatwa katika nyumba hiyo. Wengine wawili walipatikana wakiwa wamejificha kwenye vifusi na wengine wawili, akiwemo mwanamume mmoja aliyekuwa amekodisha nyumba hiyo walikamatwa.

Polisi hawakutoa majina ya waliokamatwa.

Image caption Eneo ambalo polisi wameshambulia ni karibu na uwanja Stade de France ambako milipuko ilitokea Novemba 13.

Watu 400 walijeruhiwa kwenye mashambulio hayo ya Ijumaa. Watu 221 kati yao bado wamo hospitalini, 57 kati yao wakiwa wamelazwa kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi.

Mataifa ya Ulaya yameendelea kuwa katika hali ya tahadhari.

Jumanne, mechi ya kirafiki kati ya Ujerumani na Uholanzi ilifutiliwa mbali muda mfupi kabla ya kuanza na ndege mbili za shirika la Air France zilizokuwa zikielekea Paris kutoka Marekani zilibadilisha njia kutokana na hatari za kiusalama.

IS walisema walitekeleza mashambulio hayo kulalamikia operesheni ya ndege za kijeshi za Ufaransa dhidi ya ngome zake Syria, na kuahidi kushambulia zaidi.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande alisema Jumatano kwamba IS wanatishia ulimwengu wote na kwamba atatafuta “muungano mkubwa” wa kufanya kazi pamoja kuangamiza wapiganaji hao.