Wasifu wa Abdelhamid Abaaoud

Abaaoud Haki miliki ya picha AP
Image caption Abaaoud aliuawa katika operesheni ya polisi Saint Denis

Abdelhamid Abaaoud, anayedaiwa kupanga mashambulio ya Paris ni raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Morocco.

Abdelhamid Abaaoud alilelewa Molenbeek, mtaa mmoja Brussels ambao una wahamiaji wengi kutoka Uarabuni.

Mwanamume huyo wa umri wa miaka 27 alikuwa mshirika mkuu wa Salah Abdeslam, ambaye bado anasakwa na ambaye kakake Brahim alijilipua wakati wa mashambulio hayo yaliyoua watu 129 Paris.

Abaaoud aliwahi kufungwa jela Ubelgiji mwaka 2010 kwa wizi wa mabavu, pamoja na Abdeslam.

Abaaoud – ambaye kwa jina jingine anajulikana kama Abu Umar al-Baljiki – alijiunga na Islamic State mapema 2013.

Alikuwa akiishi kwenye nyumba moja Saint-Denis iliyovamiwa na polisi Novemba 18. IS walikuwa awali wamedai kwamba alikuwa Syria, na hali kwamba alipatikana huko ni ishara kwamba walijaribu kupotosha majasusi. Labda kutaka kuwazuia kumhusisha na mashambulio ya Charlie Hebdo.

Haijabainika Abaaoud alipata itikadi kali wapi. Shirika la habari la Associated Press linasema alisomea moja ya shule za upili bora zaidi Ubelgiji - Saint-Pierre d'Uccle.

Alikuwa akiwasiliana na Mehdi Nemmouche, mwanamgambo Mfaransa wa asili ya Algeria aliyewapiga risasi na kuwaua watu wane katika makavazi moja ya Kiyahudi mjini Brussels Mei 2014.

Nemmouche pia aliishi kwa muda Molenbeek, eneo ambalo maafisa wa Ubelgiji wanakiri itikadi kali za Kisalafi zimekuwa zikisheheni miongoni mwa vijana wa Kiislamu.

Maafisa wa Ubelgiji wanashuku huenda Abaaoud alisaidia kupanga na kufadhili kundi la magaidi Verviers, mashariki mwa Ubelgiji. Kundi hilo lilisambaratishwa kwenye operesheni ya polisi Januari.

Wanajihadi wawili waliuawa Verviers – ambao IS baadaye ilisema walikuwa Khalid Ben Larbi (almaarufu Abu Zubayr, 23) na Soufiane Amghar (almaarufu Abu Khalid, 26).

Katika mahojiano yaliyochapishwa katika jarida la Kizungu la kundi la IS lijulikanalo kwa jina Dabiq mwezi Februari, Abaaoud alizungumzia kisa hicho cha Verviers.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Abaaoud alimshawishi kakake wa miaka 13 kujiunga naye Syria

Alisema alirejea kisiri Ubelgiji na wawili hao na wakatengeneza nyumba salama ambayo walitumia kutekeleza mashambulio.

“Majasusi walinijua kutoka awali kwani walikuwa wamenifunga jela,” alisema, na kujitapa kwamba bado alifanikiwa kuponyoka baada ya shambulio hilo Verviers.

"Hata nilisimamishwa na afisa wa polisi ambaye aliniangalia kwa makini na akataka kunilinganisha na picha (ya mshukiwa aliyesakwa), lakini aliniruhusu niende, hakuona tulishabihiana! Hii ilikuwa zawadi ya Allah.”

Video ya propaganda ya IS 2014 ilimuonyesha Abaaoud akiwa kwenye gari akionyesha miili iliyokuwa imewekwa sehemu ya nyuma ya gari hilo.

Abaaoud pia alihusishwa na shambulio lililotibuliwa kwenye gari moshi la Thalys Agosti mwaka huu.

Mwanamgambo, Ayoub El-Khazzani, alizidiwa nguvu na abiria kwenye gari moshi hilo kaskazini mwa Ufaransa.

Abaaoud alitajwa kama mshukiwa, sawa na shambulio katika kanisa moja Villejuif, Ufaransa.

Alikuwa amejitolea sana katika itikadi zake hivi kwamba alimshawishi kakae mdogo wa umri wa miaka 13 ajiunge naye Syria.