Raia wa Mexico wanaihama Marekani

Mexico
Image caption Kwa miaka mingi, raia wengi wa Mexico wamekuwa wakihamia Marekani

Utafiti ulioendeshwa nchini Marekani unaonyesha raia wengi wa Mexico wanaondoka kwenye taifa hilo kubwa zaidi ulimwenguni ukilinganisha na idadi ya wanaoingia nchini humo, tofauti na hali ilivyokuwa nusu karne iliyopita.

Utafiti huo uliofanywa na kituo cha utafiti cha Pew umeeleza kwamba katika kipindi cha miaka mitano mfululizo mpaka kufikia mwaka wa jana, inakadiriwa Wamexico milioni moja wakiwa na familia zao wameondoka nchini Marekani na kurejea nchini Mexico.

Katika kipindi kama hicho Wamexico 870,000 waliondoka nchini mwao kuelekea Marekani kutafuta makazi bora, idadi hiyo ikiwa chini ya waliorejea kwa 140,000.

Kituo cha Pew kinasema sababu kubwa ya kurejea nyumbani kwa Wamexico, ni ile hamu ya kutaka kuungana na familia zao.

Ripoti hii imetolewa wakati huu ambapo wimbi la wahamiaji kuingia nchini humo likiwa limeongezeka katika kampeni za urais nchini Marekani.

Mgombea mmoja kutoka upande wa chama cha Republican, Donald Trump, ametoa wazo la kujengwa kwa ukuta kati ya Mexico na Marekani kwa misingi ya kuzuia uhalifu unaofanywa na wa Mexico pamoja na usafirishaji dawa za kulevya kutoka Mexico na kuziingiza Marekani.