Wachimbaji migodi waliookolewa wakosa mali

Robi
Image caption Familia ya Robi ilifanya matanga baada ya matumaini yake kupatikana akiwa hai kufifia

Wachimbaji migodi waliookolewa baada ya kukaa chini ya ardhi siku 41 wanakabiliwa na kizungumkuti baada yao kugundua jamaa walirithi mali yao.

Walikwama katika mgodi wa dhahabu wa Nyangalata wilaya ya Kahama, mkoa wa Shinyanga walipokuwa wakijaribu kuwaokoa wenzao 11.

Mmoja wa wachimbaji hao watano aliambia mwandishi wa BBC Sammy Awami kuwa kakake alirithi viatu vyake na mali nyingine.

Mwingine alisema familia yake hata ilifanya matanga na mkewe akaondoka nyumbani.

Waliishi siku hizo zote kwa kula mizizi, mchanga, vyura na mende.

Juhudi za kuwaokoa zilisitishwa wiki moja baada yao kufunikwa na vifusi baada ya matumaini ya kuwapata wakiwa hai kudidimia.

Lakini sauti zao hafifu zilisikika na wachimbaji wengine waliokuwa wakifanya kazi karibu na eneo hilo na juhudi za uokoaji zikarejelewa.

Wachimbaji hao ni miongoni mwa waliokaa muda mrefu zaidi chini ya ardhi wakiwa hai.

Nchini Chile, wachimbaji 33 waliokolewa baada ya kusaa siku 69 ardhini mwaka 2010.

Joseph Burule Robi ambaye ni baba wa watoto wane, aliambia BBC kwamba familia yake ilifanya matanga na mkewe akarejea kwao Mwanza.

"Alijua tayari ashampoteza mumewe,” anasema Robi, 44, ambaye nyumbani kwao ni Ilemela, Mwanza.

Image caption Muhangwa anasema maisha yake duniani sasa ni kama ya mtoto mchanga

Amos Muhangwa, 25, kutoka Wamashimba, Mwanza naye anasema maisha yake duniani sasa ni kama ya mtoto mchanga kwani hamiliki chochote.

Msafiri Gerard, 38, ambaye ni baba wa watoto saba anasema viatu vyake vilirithiwa na kakake baada ya jamaa zake kuamini alikuwa amefariki.

"Siwezi kwenda kumdai kakangu na kumtaka anirejeshee viatu alivyochukua kama urithi.

“Nilidhaniwa kuwa nilikuwa nimefariki, na kwa hivyo familia yangu ilikuwa na haki kugawana mali yangu,” alisema, Gerald anayetoka Kaingesa mkoa wa Rukwa.

Tobias Uruothi anasema alipopokea simu ya kumjulisha kwamba kakake Onyiwa Kaindo, kutoka Bumera, mkoa wa Tarime, alikuwa amepatikana akiwa hai, alidhani anadanganywa na akakata simu.

Wachimbaji migodi hao hawakuwapata wenzao 11 waliokuwa wameenda kuwatafuta, na polisi wanaamini wamefariki.