Kenya na Tanzania zafuta machozi Cecafa

Image caption Kenya walitawala mechi hiyo

Kenya na Tanzania zilifuta machozi ya kubanduliwa kutoka mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa kuandikisha ushindi mechi zao za kwanza Cecafa nchini Ethiopia.

Harambee Stars walishangaza Uganda Cranes kwa kuwakomoa 2-0 katika Kundi B Jumapili mabao ua Kenya yakifungwa na Jacob Keli na Michael Olunga kwenye mechi iliyochezewa Addis Ababa.

Kinyume na Tanzania na Kenya, Uganda walisonga mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya kuwabandua Togo.

Ushindi huo ulikuwa na maana zaidi kwa mkufunzi wa Kenya Bobby Williamson kwani alikuwa kocha wa Uganda awali na akawasaidia Cranes kushinda kombe hilo.

“Ni vizuri kuanza dimba kubwa hivi kwa ushindi,” alisema.

Uganda, ambao wameshinda Kombe la Cecafa mara 13, wanashika mkia Kundi B.

Kenya wanaongoza kundini huku Burundi, waliolaza Zanzibar 1-0 Jumamosi wakiwa nambari mbili.

Katika mechi ya awali Jumapili, Tanzania walinyenyekeza Somalia kwa kichapo cha 4-0 Kundi A mabao ya Tanzania yakifungwa na John Bocco na Elias Maguli, mawili kila mmoja.

Tanzania wanaongoza kundi hilo.

Leo mechi zitakuwa mjini Bahir Dar ambako Sudan Kusini watakutana na Djibouti nao Malawi wapambane na Sudan Kundi C.