#TellThePope: Ujumbe wa Wakenya kwa Papa Francis

Wakenya mtandaoni wamekuwa wakituma jumbe zao kwa Papa Francis kuhusu yale anayofaa kufahamu kupitia kitambulisha mada #TellThePope.

Baadhi wanatumia kitambulisha mada hicho kueleza kuhusu mambo mabaya ambayo yamekuwa yakitendeka Kenya miongoni mwao ufisadi, wizi na chuki za kikabila.

Lakini kunao wanaotumia ukumbi huo kumjulisha Papa Francis kuhusu mambo mazuri anayoweza kuyapata nchini Kenya.

Ucheshi nao si haba huku taifa linapojiandaa kumkaribisha kiongozi huyo wa kanisa Katoliki duniani, mfano huyu anayemkumbusha kwamba nyasi iliyopandwa barabara ya Uhuru Highway haikupandwa kwa ajili yake. Hii inatokana na hali kwamba nyasi hiyo, iliyopandwa kabla ya ziara ya Rais Obama ilikuwa haijaota wakati kiongozi huyo wa Marekani alizuru Kenya Julai.

Wengine wanamtahadharisha kuhusu mvua kubwa ya El Nino inayoendelea kunyesha Afrika Mashariki, na kumtaka asisahau kubeba mwavuli.

Kunao wanaokerwa na wahubiri wa uongo, na ikizingatiwa kwamba ndiye kiongozi wa Kanisa Katoli duniani, wameonelea heri kumjulisha kuhusu wahubiri hawa.

Papa Francis anatarajiwa kutua nchini Kenya Jumatano Novemba 25 na baadaye kuzuru Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati.