Wamisri waua wasudan 5 mpakani

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Maafisa wa kulinda mipaka wa Misri wameua waafrika 6

Maafisa wa mpakani wa Misri wamewauwa wahamiaji 5 wa Sudan na kuwajerihi wengine 6 .

Kulingana na taarifa ya wanajeshi, Ufyatulianaji wa risasi ulianza majira ya asubuhi wakati kundi la wahamiaji kutoka Sudan wanaoarifiwa kuwa walisaidiwa na wahalifu walikaidi agizo la maafisa wa mipakani la kusimama.

Maafisa wa mpakani wa Misri walianza kufyatua risasi hewani kama onyo kwa wahamiaji waliokuwa wakielekea Israeli.

Hata hivyo kundi hilo lilianza kufyatua risasi pia na kumuumiza afisa mmoja.

Makabiliano yalianza na ni hapo raia watano wa Sudan walikopoteza maisha yao, sita wengine wakaachwa na majeraha huku watano wakitiwa mbaroni.

Mapema hii leo, maafisa wa usalama pamoja na maafisa wa afya walisema miili ya wahamiaji 6 kutoka Sudan waliouwawa ilipatikana kwenye rasi ya Sinai karibu na mpaka wa Israeli.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Tarehe 15 mwezi huu, miili 15 ya wahamiaji kutoka Afrika ilipatikana kwenye mpaka wa Israeli baada ya kupigwa risasi.

Aidha wanasema 11 wengine waliachwa na majeraha ya risasi baada ya jaribio lao la kuvuka mpaka kutibuka.

Rasi ya Sinai, ni mahali ambapo vita vimepamba moto kati ya serikali ya misri na makundi ya kigaidi, na sasa imekuwa njia kuu ya wahamiaji kutoka bara Afrika, kuingia katika taifa hilo la wayahudi.

Tarehe 15 mwezi huu, miili 15 ya wahamiaji kutoka Afrika ilipatikana kwenye mpaka wa Israeli baada ya kupigwa risasi.

Kati ya mwaka wa 2009 na 2011, maafisa wa mipakani kutoka Misri wamekuwa wakiwauwa wahamiaji kwa kuwapiga risasi, wakati wakijaribu kuvuka mpaka hadi Israeli.

Upande wa kaskazini mwa rasi ya Sinai, imekuwa ngome ya makundi ya kijihadi, tangu wanajeshi wapindue serikali ya rais Mohammed Morsi.