Ziara za awali za mapapa Kenya

Papa Haki miliki ya picha AP
Image caption Papa John Paul II alizuru Kenya mara tatu

Taifa la Kenya limekua mwenyeji wa Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani mara tatu, ziara zote zikifanywa na Papa John Paul wa Pili. Mara ya kwanza Papa John Paul kuzuru Kenya ilikua mwaka 1980. Katika ziara hii iliyoanza Mei 5, 1980, Papa alitua mjini Nairobi kutayarisha taifa na kuongoza kongamano kuu la kimataifa la imani Katoliki.

Kongamano hili hushirikisha viongozi wa kanisa Katoliki ikiwa ni pamoja na Makadinali, Maaskofu, Makasisi na waumuni wa imani hii. Ni kongamano ambalo hufanyika kwa siku kadhaa kusherehekea Yesu Kristo kama anavyojitokeza kwenye Ekarestia takatifu, hii ni kuambatana na imani Katoliki.

Katika ziara hii Papa John Paul wa Pili alizuru mataifa mengine ya Afrika ikiwa ni pamoja na Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) na Ivory Coast. Mwaka wa 1985, Kenya iliteuliwa kama mwenyeji wa Kongamano la 43 la Kimataifa la kusherekea imani Katoliki.

Agosti Mwaka huo Kongamano la kimataifa la kusherekea msingi wa Familia na imani Katoliki (Eucharist and Family Congress) liliadhimishwa mjini Nairobi mbele ya umati wa zaidi ya waumini 200,000. Kando na kuhudhuriwa na viongozi wa kidini, viongozi wa taifa akiwemo aliyekua Rais wa Kenya Daniel Arap Moi walijumuika na waumini wa imani Katoliki kwa sherehe hiyo maalum.

Baada ya kanisa Katoliki kuidhinisha mageuzi muhimu yaliyojulikana kama Vatican Council 2, hii ilitoa nafasi kwa waumini kufanya ibada zao wa kizingatia baadhi ya mila na utamaduni, kwa mfano kupiga makofi, kufanya ibada kwa kutumia lugha za mama na kuwakubalia baadhi ya waumini kusaidia kuongoza ibada. Makao Makuu ya Vatican yalitangaza kwamba Papa John Paul II atazindua Synod ya Afrika kuwapa nguvu viongozi wa kanisa Afrika kusimamia kanisa katoliki kwa misingi ya Kiafrika.

Awali wengi waliokua viongozi wa kanisa Afrika walikua Wanamishenari kutoka Bara Ulaya. Septemba 19 mwaka 1995, Papa John Paul wa pili aliongoza Sherehe ya Kanisa Katoliki Afrika, katika bustani ya Uhuru mjini Nairobi. Ni ibada iliyohudhuriwa na zaidi ya watu 300,000.

Makadinali na Maaskofu kutoka Bara Afrika walikusanyika mjini Naoribi kwa ibada hii ambayo walitunukiwa mamlaka ya kuongoza imani Katoliki Barani.

Aidha kwenye ibada hii mavazi ya waliyovalia viongozi wa kanisa Katoliki akiwemo Papa yalikuwa ya Kiafrika. Makasisi walipewa uwezo wa kutoa baraka zao kama walivyofanya mababu wa Kiafrika wakati wakifanya ibada zao.

Kwenye ziara zote alizofanya Papa John Paul wa Pili nchini Kenya, alikutana na viongozi wa imani nyingine ikiwa ni pamoja na Waislamu, Wahindi na Wakristo wengine ambao sio Wakatoliki na wanaofuata imani za kijadi.

Kila alipokanyaga ardhini alibusu udongo ambao baadaye uliwekwa kwenye kikapu. Hakupenda kutunukiwa shada la maua ila alibariki ardhi aliyokanyaga ili kuwepo na ustawi na amani.

Katika ziara zote tatu, Papa John Paul wa pili alizuru Kenya kama kiongoni wa Kanisa Katoliki duniani na pia kama Rais wa Vatican.