Polisi mzungu ashtakiwa kwa kuua tineja mweusi

Haki miliki ya picha Policia Chicago
Image caption Polisi huyo alimfyatulia risasi 16 bila tishio la maisha yake

Hofu ya kutibuka kwa mzozo wa ubaguzi wa rangi umetanda mjini Chicago Marekani baada ya idara ya polisi kufichua video moja inayoonesha mauaji ya tineja mmoja na askari mzungu.

Yamkini askari huyo alimfyatulia tineja huyo risasi 16 punde baada ya kumfumania akitoboa gurudumu la gari la polisi.

Video hiyo inayotisha, inaonesha afisa huyo Jason Van Dyke akimpiga risasi Laquan McDonald, mwenye umri wa miaka 17.

Kiongozi wa mashtaka wa jimbo hilo Anita Alvarez anasema kuwa video hiyo inaonesha afisa huyo akishuka kutoka kwa gari lake na kumfyatua risasi kadhaa kwa mvulana huyo ambaye alikuwa anatembea kutoka kwenye eneo la tukio.

''Kwa hakika inahuzunisha kuona maisha ya tineja kama huyo akipoteza maisha yake kwa uovu kama huu'' alisema Alvarez.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Afisa aliyemuua tineja mweusi Jason Van Dyke ameshtakiwa kwa kukusudia kuua

Bila shaka watu wetu wa Chicago watakapoiona video hiyo watakasirishwa sana na kuendelea kwa matukio ya utumizi mbaya wa silaha dhidi ya watu weusi haswa kutoka kwa maafisa wa usalama wazungu.

Video hiyo iliyopigwa na kamera iliyokuwa imetundikwa kwa gari lingine la polisi inamuonesha kijana huyo McDonald akikimbia barabrani kisha alipowaona maafisa wa polisi Van Dyke na mwenzake akageuka mara moja akainua suruali yake kisha akaanza kutembea kwa kwasi kuondoka kwenye eneo la tukio.

Mara moja anavurumishwa juu na kuangushwa chini na milipuko ya risasi kadhaa.

McDonald anajaribu kuinua kichwa chake lakini risasi zaidi zinambana chini

Haki miliki ya picha AP
Image caption Makumbusho ya Laquan McDonald

Analala hapo chini akivuja damu na hakuna afisa anayekwenda kumsaidia kuokoa maisha yake.

Kiongozi wa mashtaka anasema kuwa Van Dyke alifyatua risasi sekunde 30 baada ya kuwasili katika eneo la tukio huku na sekunde 6 tu baada ya kushuka kutoka kwa gari lake.#

Bila shaka hakuchukua muda wake kupeleleza hali halisi katika eneo la tukio.

Hii ndio mara ya kwanza kwa afisa anayehudumu kufunguliwa mashtaka ya kuua akikusudia.

Jason Van Dyke anashtakiwa kwa mauaji ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 17 Laquan McDolald mwezi Oktoba mwaka uliopita.