Marekani ilishambulia kliniki 'kimakosa'

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wafanyikazi wa kliniki ya Kunzu Afghanistan

Ndege moja ya kijeshi ya Marekani iliishambulia kliniki moja ya shirika la madaktari wasio na mipaka la Medicine San Frontieres MSF katika mji wa Afghanistan wa Kunduz kutokana na makosa ya kibinaadamu.

Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa wanajeshi waliokuwa katika ndege hiyo ya AC-130 walikosea kwa kudhani kliniki hiyo ilkuwa jengo la serikali lililotekwa na wapiganaji wa Taleban.

Takriban watu 30 walifariki katika shambulizi hilo la Oktoba 3, katika harakati za kuuchukua mji wa Kunduz kutoka kwa wapiganaji wa Taliban.

MSF imeelezea mashambulizi hayo kama uhalifu wa kivita na kutaka uchunguzi mwafaka kufanywa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kliniki ya MSF Kunduz

Shirika hilo la matibabu ya hisani pia lilipinga maoni ya awali ya Marekani kuhusu shambulizi hilo,yaliodai kwamba vikosi vya Marekani vilitekeleza shambulizi karibu na hospitali hiyo kwa kuwa vilikuwa vikishambuliwa.

Jeshi la Marekani baadaye lilikiri kwamba shambulizi hilo lilikuwa la kimakosa na kuanzisha uchunguzi.