NATO yaikinga kifua Uturuki

Haki miliki ya picha

Jumuia ya kujihami ya nchi za magharibi NATO imesema inasimama pamoja na Uturuki baada ya kuitungua ndege ya kivita ya Urusi.

Akizungumza baada ya mkutano wa dharura ulioitishwa na Uturuki, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema tathmini ya tukio hilo inaonyesha kuwa ndege ya kivita ya Urusi iliruka katika anga ya Uturuki.

Huku kukiwa na hali ya wasiwasi, Stoltenberge ametaka kuwepo na hali ya utulivu kutoka pande zote.

Amesema taarifa walizozipokea kutoka nchi washirika, zinaenda sambamba na maelezo ya Uturuki ya tukio hilo.

"Ushirikiano tulioupata kutoka kwa washirika mbalimbali kwa leo unathibitisha taarifa tuliyoipata kutoka Uturuki."

Hata hivyo, Moscow bado wanasisitiza kwamba, ndege hiyo ilikuwa katika anga ya Syria, na kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa anga ya Uturuki.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema kila mtu sharti aheshimu haki ya nchi yake ya kulinda mipaka yake.

Rais Obama pia ameitetea haki ya Uturuki ya kulinda anga yake.

Kwa upande wake, msemaji wa jeshi la Urusi, Jenerali Sergey Rudskoi, amesema angalau rubani mmoja kati ya wawili wa ndege hiyo iliyoangushwa na Uturuki siku ya Jumanne amefariki kutokana na moto uliokuwepo chini baada ya kutoka katika ndege hiyo.

Mpaka sasa hakijulikani kilichomsibu rubani mwengine.