Hotuba ya kwanza ya Papa Francis Afrika

Papa Ziara
Image caption Papa Francis ameeleza hamu kubwa ya kukutana na vijana wakati wa ziara yake

Papa Francis ametoa hotuba yake ya kwanza baada ya kutua Kenya akihimiza umoja, kuwathamini vijana na kuyatunza mazingira.

Hii hapa hotuba hiyo kamili ambayo ameitoa akiwa Ikulu ya Nairobi:

Nashukuru sana kwa kunikaribisha vyema, kwenye ziara yangu ya kwanza Afrika. Nakushukuru Bw Rais, kwa maneno yako yenye ukarimu kwa niaba ya Wakenya, na nasubiri kwa hamu kukaa kwangu hapa.

Kenya ni taifa changa na linalokua na lenye jamii mseto na limekuwa likitekeleza jukumu muhimu kanda hii. Kwa njia nyingi, mnayopitia katika kuunda demokrasia yamekuwa yakipitiwa na mataifa mengi Afrika.”

Sawa na Kenya, mataifa hayo mengine pia yanajizatiti kuunda, juu ya msingi wa kuheshimiana, maridhiano na ushirikiano, jamii yenye makabila nyingi, ambayo ina uwiano, ni ya haki na inajumuisha wote.”

Taifa lenu pia lina vijana wengi. Siki hizi nitakazokuwa hapa, nasubiri sana kukutana na wengi wao, kuzungumza nao na kuwapa matumaini katika ndoto zao za siku za usoni.”

Vijana ndio rasilimali yenye thamani zaidi kwa taifa. Kuwalinda, kuwekeza katika vijana, na kuwasaidia, ndiyo njia bora zaidi ya kuhakikisha siku njema za usoni zenye kufuata busara na maadili ya kiroho ya wazee wetu, maadili ambayo ndiyo nguzo ya jamii.

Kenya imebarikiwa sio tu na umaridadi, katika milima, mito na maziwa, misitu, nyika na maeneo kame, bali pia katika utajiri wa maliasili. Wakenya wamethamini sana zawadi hizi kutoka kwa Mungu na wanajulikana kwa utamaduni wao wa kuhifadhi (mazingira). Mgogoro wa kimazingira unaokumba dunia kwa sasa unahitaji kutambua zaidi uhusiano kati ya binadamu na maumbile.

Tuna wajibu wa kupitisha maumbile haya yakiwa hayajaharibiwa kwa vizazi vijavyo. Maadili haya yamekuwepo kwenye jamii za Kiafrika.

Kwenye ulimwengu ambao

Katika ulimwengu ambao unaendelea kutumia tu badala ya kulinda mazingira, lazima tuhimize viongozi wetu wa kitaifa kuendeleza mifumo ya kuwajibika ya maendeleo ya kiuchumi.

Kuna uhusiano wa moja wa moja kati ya kulinda mali asili na kujenga mfumo wa kijamii wa haki na usawa.

Hakuwezi kukatokea kufanywa upya kwa uhusiano kati yetu na maumbile bila kufanywa upya kwa ubinadamu wenyewe.

Jamii zetu zinapoendelea kukumbwa na migawanyiko, ya kikabila, kidini au kiuchumi, binadamu wote wenye nia njema wameitwa kufanyia kazi maridhiano, msamaha na uponyaji. Katika juhudi za kuunda mfumo wa demokrasia, kuimarisha utangamano na uwiano, kuvumiliana na kuheshimiana, lengo kutenda mema linafaa kuwa ndilo kuu.”

Historia inaonyesha kuwa ghasia, mizozo na ugaidi huchochewa na kuogopana, kutoaminiana na kutamauka ambako husababishwa na umaskini na kupoteza matumaini. Vita dhidi ya maadui wa amani na ustawi vinafaa kuendeshwa na wanaume na wanawake wanaoamini katika, na kushahidia, maadili makuu ya kidini na kisiasa ambayo yalipelekea kuasisiwa kwa taifa.

Mabibi na mabwana, kuendelezwa na kulindwa kwa maadili haya ni jukumu lenu, viongozi wa kisiasa, kitamaduni na kiuchumi wan chi. Huu ni wajibu mkuu, wito kamili, kutumikia Wakenya wote. Injili inatwambia kwamba kutoka kwa aliyepewa mengi, mengi zaidi yatadaiwa (Lk 12:48). Kwa moyo huo, nawahimiza kufanya kazi kwa maadili na uwazi kufanikisha mema na kuendeleza umoja katika kila ngazi ya jamii.

Nawahimiza sana kuwajali maskini, ndoto za vijana, na kugawana vyema maliasili na nguvu kazi ambazo Mola amelipa taifa lenu. Nawahakikishia kuendelea kwa juhudi za kanisa Katoliki, kupitia kazi zake za elimu na kusaidia jamii, kutoa mchango katika hili.”

Mafariki wapendwa, naambiwa hapa Kenya ni kawaida watoto shuleni kupanda miti kwa ajili ya siku za usoni.

Naomba ishara hii ya matumaini katika siku za usoni, na imani katika ukuaji ambao Mungu hutoa, viwasaidie nyote katika juhudi za kuhakikisha jamii yenye mshikamano, haki na amani humu nchini na bara lote la Afrika.

Nawashukuru tena kwa kunikaribisha vyema, na kwenu na familia zenu, na watu wote wa Kenya, ziwe baraka tele za Mwenyezi Mungu.”

Mungu abariki Kenya!”