MOJA KWA MOJA: Siku ya pili ziara ya Papa Francis

Bofya hapa kupata habari za karibuni zaidi

18.42:Papa Francis akamilisha hotuba yake

Image caption Papa akiwa katika makao makuu ya umoja wa mataifa jijini Nairobi

18.41:Amesema kuwa hakuna litakalofanyika hadi pale suluhisho la kisiasa na kiufundi ziambatane na elimu ambayo inapendekeza maisha mapya na tamaduni mpya

Hatua hiyo itaafikiwa kupitia elimu inayowashirikisha watoto wa kiume na wale wa kike ,wanaume na wanawake,wadogo kwa wakubwa

18.32:Ningependa kusema kuwa kanisa katoliki litasaidia katika maombi ili kuhakikisha kuwa muungano uliopo Afrika katika maswala ya kibiashara utaangazia hali mbaya ya watoto wa bara hili.

1830:Hatuwezi kunyamaza kuhusu maswala ya biashara haramu ya usafirishaji kwa madai ya umasikini.Mauaji ya ndovu ,ghasia za kisia na ugaidi ni kilio kinachotakiwa kuangaziwa na jamii ya kimataifa.

Mkutano wa 10 wa Biashara utakaofanyika mjini Nairobi unafaa kutumiwa kuangazia maisha ya binaadamu kwa lengo ya kuyaimarisha.

Kuna muhimu wa kuhakikisha kuwa watu wengi wana uwezo wa kupata matibabu.

Kuna umuhimu wa kupanga majengo katika miji pamoja na kuangalia maisha ya wanaoishi mijini.,kwa lengo la kuimarisha maisha yao.

18.28:Maisha mengi, habari nyingi ,ndoto nyingi zimeharibiwa hatuwezi, kuangalia haya yakiendelea .Hatuna haki kufanya hivyo.

Usafirishaji wa binaadamu,kazi za lazima ukahaba ni sharti kuangamizwa

18.27:Binaadamu lazima tuchagua kilicho chema na kuweka mwanzo mpya.

tunahitajji kuwa na majadiliano na wanasayasi,mataifa na mashirika ya kijamii.Ushirikiano wa ukweli kati ya siasa na sayansi huleta mafanikio mema.

18.26:Tunajukumu sote kuleta mabadiliko kupitia kutegemeana

kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anaga na kuheshimu haki za kibinaadamu.

18.15:Papa Francis ajitayarisha kuzungumza

17.58:Papa Francis kwa sasa ameingia katika ukumbi wa mikutano wa Umoja wa Mataifa mjini Nairobi huku waliohudhuria wakimshangilia kwa vifijo na nderemo.

17.57:Papa Francis tayari amewasili katika jumba la makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi.

17.50:Papa Francis atarajiwa kuzungumzia kuhusu kupanda kwa viwango vya joto duniani.Vilevile anatarajiwa kuzungumzia kuhusu Mkutano wa mabadiliko ya hali ya anga unaotarajiwa kufanyika siku chache zijazo.

17:10 Papa Francis sasa anaelekea makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mazingira (UNEP) eneo la Gigiri.

16:58 Papa Francis: "Asanteni kwa kumfuata Yesu. Tafadhali, msisahau kuniombea, kwa sababu nahitaji (maombi).

16:57 Papa Francis: "Nawaacha na swali moja. Huwa napunguza muda wangu wa kulala? Muda wa kuangalia televisheni, redio, kuomba? Au napenda hizo? Jiwekeni mbele ya yesu aliyeanza kazi iliyo ndani yenu na anayeendelea. kwa maombi. Neno la mwisho ningependa kuwaambia - kabla ya kusema jingine - ni, ni kwamba kila mtu aliyeteuliwa na Yesu ni wa kutoa huduma. Kuhudumia watu wa Mungu. Kutumikia maskini, wale waliotengwa, kutumikia watoto. Wale ambao hata hawafahamu fahari iliyo ndani yenu. Jiacheni mtumiwe na Yesu, muwe huru kutoa huduma, si kuhudumiwa. Mwaka mmoja hivi uliopita, kulikuwa mkutano wa mapadri, watawa mko huru sasa, na wakati wa shughuli za kiroho, kila siku kulikuwa na zamu kwa padri kutumikia mezani. Baadhi walikataa, na kusisitiza kwamba wahudumie. Kwamba waliingia kwenye huduma watumikiwe. Msiwe hivyo. Msiache mhudumiwe, hudumieni wengine."

16:54 Papa Francis: "Padri asiyeomba, ana moyo usiovutia."

16:52 Papa Francis: "Msijitenge na Yesu. Hii ina maana kwamba msiache kamwe kuomba. Wakati mwingine ni vigumu, unapolala, basi ni vyema basi, lala mbele ya Mungu, ni njia ya kuomba. Lakini kaa hapo, mbele ya Mungu. Usiondoke."

16:48 Papa francis: "Mkakumbuka Injili wakati James alilia? Au John? Au mtume mwingine? Ni mmoja tu aliyelia. Yule aliyegundua alikuwa mkosefu. Kwamba alimsaliti Bwana wake. Na alipogundua hilo alilia. Na Yesu alimfanya Papa. Nani anamwelewa Yesu huyu? Usiache kulia. Padri, mhudumu wa kiume au kike, anapolia, kwa makosa yake, kwa uchungu duniani, kwa watu wanaoteseka, wazee, waliotengwa. Lilia watoto walioauawa. Kwa yale tusiyofahamu. Tulie tunapoulizwa Ni Kwa Nini? Hakuna hata mmoja kati yetu ana jibu la maswali hayo yote. Kuna mwandishi, Mrusi, aliyejiuliza mbona watoto huteseka? Na kila ninapokutana na watoto wagonjwa sana, huwa najiuliza, ni kwa nini? Na sina majibu. Lakini huwa namwangalia Yesu. Kuna mambo duniani yanayotulazimu kulia na kumwangalia Yesu. Na hiyo ndiyo njia pekee ya kuchukulia baadhi ya mambo."

16:47 Papa Francis: "Aliyeanza kazi nzuri ataendelea kuikamilisha. Hili hutupa msukumo."

16:39 “Nawashukuru kwa mchango wenu kwa Kanisa na kwa jamii ya Kenya – watu wengi waliotawazwa, na mapadri. Nawaomba mfikishe salamu zangu kwa ndugu na dada ambao hawakuweza kuungana nasi, hasa waliozeeka na walio wagonjwa.”

16:37 Papa Francis anaanza kuhutubia makasisi, watawa na wanamishenari wa Kanisa Katoliki katika shule ya St Mary's. Amesema hana ufasaha sana wa kunena kwa kutumia Kiingereza, lakini atatumia Kihispania. Hotuba yake inatafsiriwa na mkalimani.

15:51 Anakaribishwa kwa wimbo "Ni baraka kutoka kwa Mungu"

15:45 Papa Francis amewasili uwanja wa shule ya St Mary's, Nairobi.

14:50 Hivi ndivyo hali ilivyokuwa watu wakisafiri kufika uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi kuhudhuria ibada iliyoongozwa na Papa Francis.

Huwezi kusikiliza tena

12:17 Waumini wameendelea kuondoka uwanjani baada ya kumalizika kwa ibada ya misa. Papa Francis amepangiwa kukutana na makasisi, watawa na waseminari katika shule ya St Mary’s, Nairobi mwendo wa saa kumi kasorobo. Baadaye atazuru makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mazingira (UNEP).

Baadhi ya waumini walikuwa wamekaa barabarani wakitarajia pengine Papa Francis angepitia na wapake fursa ya kumsalimia.

11:40 Ibada ya misa inamalizika. Waumini hata hivyo wanaendelea kupokea komunyo.

11:28 Kadinali Njue: Asante kwa kuwa nguzo ya umoja wetu na kwa kusaidia kukabili masuala yanayoathiri binadamu, jambo linalotufanya kutafakari na kubadilisha maisha yetu.

11:25 Kadinali John Njue anazungumza kwa sasa. Ametoa shukrani kwa Papa Francis kwa kukubali mwaliko wa Kanisa Katoliki Kenya na kuzuru Kenya kama taifa lake la kwanza kabisa barani Afrika.

10:47 Sasa ni wakati wa kutoa sadaka kwenye ibada ya misa inayoongozwa na Papa Francis uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

10:44 Ni wakati wa maombi. Waumini wanaomba kwa lugha za Kiafrika.

10:36 Papa Francis akamilisha mahubiri yake kwenye ibada ya misa uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi. Amemalizika kwa kusema: "Mungu abariki Kenya!"

10:05 Hivi ndiyo yasemavyo baadhi ya magazeti ya Kenya kuhusu ziara ya Papa Francis ambaye aliwasili Kenya jana.

10:00 Ibada ya misa inayoongozwa na Papa Francis uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi imeanza. Viongozi wakuu akiwemo Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga amehudhuria ibada hiyo.

09:38 Papa Francis amewasili katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi ambako natarajiwa kuongoza ibada ya misa dakika chache zijazo.

09:10 Papa Francis ameondoka Lavington baada ya kukutana na viongozi wa kidini na sasa anatarajiwa kuelekea Chuo Kikuu cha Nairobi ambako ataongoza ibada ya misa mwendo wa saa nne.

09:05 Papa Francis: "Ninaamini Mungu ni Mungu wa amani. Jina lake takatifu halifai kutumiwa kutetea chuki na mauaji. Ninajua kwamba mashammbulio ya Westgate, Chuo Kikuu cha Garissa na Mandera bado hayajasahaulika. Na sana, vijana wamekuwa wakiingizwa na kufunzwa itikadi kali kwa jina la jini kupanda woga na kuvunja umoja katika jamii. Ni muhimu sana tuwe manabii wa amani, watu wa amani wanaokaribisha wengine kuishi na amani, umoja na kuheshimiana. Mungu na akaguze nyoyo za wanaohusika katika mauaji na ghasia, na azipe imani familia na jamii zetu."

09:00 Papa Francis: "Huwa ni muhimu sana kwangu kwamba, ninapofika pahali kutembelea waumini wa kanisa Katoliki, ninakutana na viongozi wa makanisa mengine na dini nyingine. Natumai kuwa wakati ambao tumekuwa pamoja utakuwa ishara ya matamanio ya Kanisa kwa dini zote, ninaomba ikaweza kuimarisha urafiki ambao tayari tunajivunia."

08:58 Papa Francis amesema anatumai ziara yake itaimarisha uhusiano kati ya dini mbalimbali.

08:47 Papa Francis kwa sasa anakutana na viongozi wa kidini afisi ya mwakilishi wa Papa Nairobi, mtaa wa Lavington. Miongoni mwa viongozi wa makanisa mengine waliohudhuria ni kiongozi wa Kanisa la Kiangilikana Kenya Dkt Eliud Wabukala. Viongozi wa dini ya Kiislamu Kenya pia wamehudhuria mkutano huo, wakiongozwa na Prof Abdulghaful El-Busaidy.

08:44 Mapadri pia wamejitokeza kwa wingi na baadhi wanashiriki katika kuandaa ibada. Wengine tayari wameketi katika viti vyao.

08:27 Usalama umeimarishwa ndani ya uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi na hata nje.

Angani kuna ndege ambayo imeonekana ikizunguka juu ya jiji la Nairobi.

08:00 Watawa nao pia wamejitokeza kwa wingi kuhudhuria ibada hiyo.

07:46 Wanafunzi kutoka shule mbalimbali wamealikwa kuhudhuria na wamefika wakiwa wamevalia sare zao.

07:41 Nairobi mvua imekuwa ikinyesha asubuhi lakini hilo halijawazuia watu kujitokeza. Tayari baadhi wamefika na kuketi kwenye viti wakiwa wanajikinga mvua kwa kutumia miavuli.

07:35 Watu wanaopanga kuhudhuria ibada hiyo walianza kufika katika uwanja wa chuo hicho mapema asubuhi. Foleni ndefu zimeshuhudiwa hata kabla ya jua kuchomoza.

07:31 Hujambo! Leo ni siku ya pili ya ziara ya Papa Francis aliyewasili Nairobi jana na miongoni mwa mengine anatarajiwa kuongoza ibada ya misa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi saa nne.

Karibu tukupashe.

Image caption Jukwaa ambalo Papa Francis anatarajiwa kutumiwa wakati wa misa