Ripoti yaonyesha ubadhirifu wa fedha A Kusini

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, mkaguzi mkuu Kimi Makwetu alisema taifa la Afrika Kusini lilipoteza zaidi ya dola milioni 65 katika kipindi cha makadirio ya pesa za uma cha mwaka 2014-2015, kutokana na matumizi mabaya katika mwaka uliotangulia.

Makwetu alisema kwamba, ili idara zote za serikali ziimarishe huduma zake, sekta tatu muhimu lazima zirekebishwe.

Sekta hizi ni elimu, afya na huduma za uma.

Hizi ndizo sekta zinazochukua fedha nyingi za bajeti ya taifa, lakini kwa mujibu wa Makwetu, idara hizi muhimu zimeshindwa kuwajibika vilivyo katika matumizi ya pesa za uma.

Katika uchunguzi wake, mkaguzi mkuu pia alisisitiza kwamba hakuna uongozi imara wa kukabiliana na ufujaji wa mali ya uma.

Kwa upande wake, rais Jacob Zuma alisema yafaa wahusika wawajibike katika usimamizi m'baya wa mali ya uma.

Wadadisi wa mambo wanasema matumizi mabaya ya pesa za uma yanasikitisha huku ukuaji wa uchumi ukilemazwa. Wizara ya fedha ya Afrika Kusini imeahidi mikakati mahsusi ya kuthibiti bajeti ya taifa