MOJA KWA MOJA: Siku ya tatu ya Papa Kenya

Bofya hapa kupata habari za karibuni zaidi

16:14 Ndege iliyombeba Papa Francis yapaa kutoka uwanja wa ndege wa JKIA, Nairobi na kuelekea Entebbe nchini Uganda.

15:52 Papa Francis aingia kwenye ndege yake, ya shirika la Alitalia. Awapungia watu mkono kuwaaga.

15:40 Papa Francis kwa sasa yuko uwanja wa JKIA, Nairobi akijiandaa kuondoka kuelekea Uganda.

15:20 Msafara wa magari ya Papa Francis unaelekea uwanja wa ndege wa JKIA.

14:50 Maandalizi ya kumuaga Papa Francis yanaendelea uwanja wa ndege wa JKIA. Papa anatarajiwa kuondoka Kenya kuelekea Uganda muda mfupi kabla ya saa kumi alasiri.

12:03 Papa Francis sasa anabariki miche ya miti iliyobebwa na vijana, kisha kuondoka kwenda kukutana na maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya.

12:01 Papa Francis: Mungu awabariki nyote! Asanteni sana.

12:01 Papa Francis: Nawashukuru, mwanzo kwamba mlifika hapa, pili mkaniruhusu nizungumze na lugha yangu ya mama, kisha mkaleta rosari, nawasihi, niombeeni. Kwa sababu nami pia nahitaji maombi. Nategemea maombi yenu. Na kabla ya kuondoka, tusimameni sasa. Tuombe pamoja kwa Baba yetu aliye mbinguni. Aliye na udhaufi mmoja, kwamba hawezi acha kuwa baba yetu. (Papa Francis anaongoza ombi la 'Baba Yetu')

Haki miliki ya picha AFP

11:57 Papa Francis: Kuna suluhu moja pekee. Kutenda hilo ambalo hukupokea. Ikiwa hakuna aliyekuelewa, basi waelewe wengine. Iwapo hukupendwa, wapende wengine. Iwapo ulihisi uchungu wa upweke, karibia walioachwa peke yao.

11:57 Papa Francis: Hii ndiyo maana familia ni muhimu. Teteeni na kulinda familia daima. Kokote, sio tu watoto wanaotelekezwa, bali pia wazee. Kuachwa bila mtu wa kuwatembelea, kuwatunza.

11:56 Papa Francis: La mwisho kutoka kwa Emmanuel "unaweza kuwaambiaje vijana wasiopata upendo katika familia zao"?

11:53 Papa Francis: Nitawaambia kitu. Ni saa sita. Mnahisi njaa? Mfukoni, daima mimi hubeba vitu viwili. Rosari kwa sababu ya kuomba, jambo ambalo linakaa la kushangaza. Na hapa, kuna historia ya kushindwa kwa Mungu, njia ya msalaba. Yesu alipoteswa, na alipohukumiwa hadi akazikwa. Kwa vitu hivi viwili, huwa nafanya kila niwezalo.

11:46 Papa Francis: Jambo la kwanza la kuzuia vijana kujiunga na makundi haya ni kuwapa elimu na kazi.

11:41 Papa Francis: Emmanuel, pia alisema mema. Nina wasiwasi na la kwanza alilosema. Ni nini tunaweza kufanya kusaidia vijana walioingizwa makundi ya itikadi kali. Twahitaji kujiuliza kwanza, mbona vijana hawa hukubali kujiunga na makundi haya?

11:40 Papa Francis, kulikuwa na swali, jinsi ya kutumia teknolojia za mawasiliano kueneza neneo la Mungu na kutenda mema. Lakini njia bora zaidi ni kutumia maneno, kuonyesha upendo kwa wengine.

11:40 Papa Francis: Ufisadi si njia ya uhai, ni njia ya mauti.

11:35 Papa Francis: Vyote mnavyoiba, vitasalia hapa, vitumiwe na wengine. Hutaenda navyo (utakapofariki).

11:35 Papa Francis: Nawasihi, msiipende sukari hiyo iitwayo ufisadi. Katika ufisadi, sawa na katika kila jambo, lazima uchukue msimamo.

11:35 Papa Francis: (Ufisadi) Ni kama sukari, tamu, twaipenda, ni rahisi. Kisha, tunaishia kuumia. Sukari zaidi hivi kwamba tunapata kisukari, au taifa letu linaishia kuwa na kisukari.

11:30 Papa Francis: Swali jingine la Linet ni ufisadi. Tunaweza kutetea ufisadi, kwa sababu eti kila mtu anapokea rushwa? Nchini mwangu, kijana wa miaka 20. Alijitolea katika siasa, alisoma kwa bidii na kutafuta kazi wizarani. Siku moja, ilimbidi kuamua ni vitu vipi angenunua. Na aliuliza bei kutoka kwa watu watatu. Aliamua kuchukua ile nafuu zaidi. Alienda kwa mkubwa wake aidhinishe, lakini akaulizwa mbona akachagua hiyo? Kwa sababu unahitaji kuchagua lile rahisi kwa wanaogharimia matumizi ya taifa. Akaambia hapana, chagua inayoweka pesa nyingi mfukoni mwako. Kijana huyo akateta, akasema nilikuja hapa kutenda mema kwa taifa. Mkubwa wake akamjibu, huwa nafanya siasa kuiba, kujitajirisha. Na si katika siasa, katika maisha yote. Hata Vatican, kuna visa vya ufisadi. Ni jambo linalouma kutoka ndani.

(Papa Francis anawasalimia vijana kadha, kisha anaendelea ha hotuba).

11:24 Linet amezungumzia ukabila. Tunafaa kusikilizana. Utamaduni wako ni upi? Mbona unapenda hili? Jana ilitajwa kuwa siku ya maombi ya kitaifa. Nawaita, tushikane mikono, tuinue kama ishara dhidi ya ukabila. Sisi sote ni taifa moja. Hivi ndivyo nyoyo zenu zafaa kuwa. Ukabila sio kushikana mikono leo tu, bali kubadili roho zetu. Tuukabili ukabila kila siku.

11:21 Papa Francis: Vijana wapendwa, hatuishi mbinguni. Tunaishi duniani na kuna shida nyingi. Sio tu matatizo, lakini pia mambo ya kuwapotosha. Lakini kuna kitu kila mmoja wenu analo. Kitu kikubwa. Uwezo wa kuamua njia ya kufuata.

11:18 Papa Francis: Kuna neno najua litauma lakini sitaki kulikwepa. Mlinionyesha neno hili mliponiletea rosari. Askofu alilitumia wakati wa maombi ya maandalizi ya siku hii. Mwanamume au mwanamke hupoteza utu anaposahau kuomba.

11:15 Papa Francis anaamka kuzungumza. Anawashukuru kwa kumpa rosari.

11:08 Emmanuel asema vijana wametenga Novemba 27 kwamba watakuwa wakipanda miti. Amuomba abariki miche michache ya miti ambayo watarudi nayo nyumbani kwenda kupanda. Anampa Papa rosari.

11:07 Emanuel Mwonga, katibu wa kundi la vijana kutoka jimbo la Machakos sasa anahutubu. Asema mashambulio ya kigaidi, baadhi yakilenga vijana, nusura yawafanye vijana wapoteze imani, lakini Papa Francis aliwapa moyo.

11:00 Bi Wambui ametaja ukabila na ufisadi kama moja ya matatizo makubwa yanayowasumbua vijana.

11:00 Katibu wa muungano wa vijana Kenya Linet Wambui anahutubia Papa kwa niaba ya vijana. Asema ziara ya Papa Francis ni baraka kubwa.

10:53 Askofu wa Jimbo la Kitui Anthony Muheria anahutubu sasa, akimkaribisha Papa Francis uwanja wa Kasarani. Asema vijana wameahidi kupanda miti na kumuomba abariki baadhi ya miti. Pia baadhi ya vitu vya kutumiwa katika maisha ya kawaida na shuleni. "Karibu Baba uzungumzie nafsi zetu, na utubariki."

Kabla ya Papa Francis kuwasili Kenya, Askofu Muheria alizungumza na BBC kuhusu matarajio ya kanisa kuhusu ziara hiyo. Pata makala hiyo hapa: Ziara ya Papa itatupatia mwamko mpya

10:45 Sasa msichana kipofu anasimama kusoma kifungu cha Biblia.

10:36 Papa Francis anaingia uwanjani sasa.

Huwezi kusikiliza tena

10:34 Kwaya ya vijana kwa sasa inatumbuiza kwa wimbo maarufu wa "Hakuna Matata".

10:20 Papa Francis awasili uwanja wa Kasarani.

10:00 Papa Francis ameondoka Kangemi na sasa anaelekea Kasarani, ambako atahutubia vijana kisha akutane na maaskofu wa Kanisa Katoliki.

09:42 Papa Francis: "Mungu awabariki! Na zaidi ya yote, nawasihi tafadhali, niombeeni."

09:42 Papa Francis: “Nawasihi, tuombe pamoja, tufanye kazi pamoja na kujitolea kuhakikisha kila familia ina makao bora, maji, choo, kawi, barabara, maeneo ya kuchezea na maeneo ya Sanaa.”

09:41 Papa Francis: “Ninawahimiza Wakristo, na mapasta wao hasa, wafanya upya juhudi zao za kimishenari, kusaidia maskini, kulinda matunda ya kazi ya maskini na kusherehekea ushindi kwa pamoja. Najua tayari mnatenda mengi, lakini naomba mkumbuke hii si kazi nyingine tu, ndiyo kazi muhimu zaidi kwa sababu, “Injili imeangazia kwa njia ya kipee watu Maskini.”

09:40 Papa Francis: “Ninapendekeza uangaziaji mpya wa kujuisha watu wote mijini kwa heshima, kinyume na mtazamo wa kuondoa watu na kutojali maskini. “Deni la kijamii na kimazingira ambalo maskini mijini wanadai linaweza kulipwa kwa kuheshimu haki zao tatu kuu “za L tatu (Kwa Kiingereza)”: Land, Lodging, Labour. (Ardhi, Malazi na Kazi). Huu ni msaada, ni wajibu wetu sote.”

09:34 Papa Francis: “Uhalisia huu ambao nimetaja hapa si visa ambavyo havihusiano hata kidogo. Ni matokeo ya aina mpya za ukoloni.”

09:32 Papa Francis: “Hali hii ya kutowajali watu wa mitaa duni huzidi hasa mapigano na ghasia vinapoenea na makundi ya wahalifu, ambayo hutumikia maslahi ya kiuchumi au kisiasa, hutumia watoto kama silaha. Pia natambua wanawake wanaopigana kwa ujasiri kulinda watoto wao dhidi ya hatari hizi. Na namuomba Mungu kwamba watawala waanze, pamoja nanyi, safari ya kufuata njia ya kujumuisha wote, kijamii, katika elimu, michezo, hatua za kijamii, na kulinda familia, kwani hii ndiyo njia ya pekee ya kuhakikisha Amani halisi na ya kudumu.”

09:31 Papa Francis:“Tatizo moja kubwa ni kuhusiana na ukosefu wa miundo mbinu na huduma za kimsingi. Namaanisha vyoo, mifumo ya maji taka, uzoaji wa taka, umeme, barabara, shule, hospitali, maeneo ya kuchezea, studio na karakana za wasanii na mafundi. Pia maji ya kunywa.”

09:29 Katika uwanja wa Kasarani, vijana wamefika kwa wingi. Mwandishi wa BBC Anne Soy yumo uwanjani.

Huwezi kusikiliza tena

09:28 Papa Francis:“Ninafahamu kuhusu tatizo kubwa linalosababishwa na “wastawishaji wa kibinafsi” wasio na sura ambao hujitwalia ardhi na hata kujaribu kunyakua viwanja vya kuchezea vya watoto wenu shuleni. Hili ndilo hufanyika tunaposahau kwamba 'Mungu aliwapa watu wote ardhi, waitumie kwa maisha yao, bila kutenga au kupendelea yeyote.'"

09:28 Papa Francis: “Kushuhudia dalili hizi za maisha mema ambazo huongezeka miongoni mwenu hata hivyo haiwezi kufanya watu wasahau ukiukaji wa haki na kutengwa kwa mitaa yenu. Vidonda hivi nyinyi hutendewa na matajiri wanaokwamilia mamlaka na utajiri, hutumia pesa kwa ulafi huku wale wengi wakilazimika kutorokea, maeneo yenye maisha duni.”

09:27 Papa Francis: “Ninawapongeza, naungana nanyi na ningependa mjue kwamba Bwana hajawasahau na huwa hawasahau daima. Njia ya Yesu aliianza kutoka pembeni, inatoka kwa maskini na pamoja na maskini, hadi kwa wengine.”

09:24 Papa Francis: "Mwanzo kabisa, hata hivyo, ningependa kuzungumzia jambo ambalo lugha ya kuwatenga watu kawaida hupuuza au huonekana kutotilia maanani. Ni busara na hekima inayopatikana katika mitaa maskini.”

09:20 Papa Francis: “Najihisi nyumbani nikiwa nanyi ndugu na dada zangu, ambao sina haya kusema, mna nafasi muhimu katika maisha yangu na maamuzi yangu. Niko hapa kwa sababu nataka mjue furaha yangu na matumaini yangu, shida zengu na mahangaiko, si tofauti na ninayopitia. Natambua matatizo mnayopitia kila siku! Ninawezake kutokashifu hali yenu kutotendewa haki?"

09:19 Papa Francis sasa anaanza kuhutubu. Anahutubu kwa Kihispania, na mkalimani anatafsiri kwa Kiingereza.

09:16 Mtawa Mary sasa anahutubu. Anazungumzia unyakuzi wa ardhi na watu wenye ushawishi. "Ziara yako inatupatia ujasiri," amesema. "Tunakuombea, na tunakutakia baraka katika kazi yako."

09:07 Kwa sasa, msichana mkazi wa mtaa duni anatoa ushuhuda kuhusu maisha yake. Anazungumzia dhuluma wanazotendewa wakazi wa mitaa duni.

08:49 Askofu Martin Kivuva anamkaribisha Papa katika kanisa hilo. Amesema ni makao ya kikundi cha Wajesuit. "Karibu nyumbani kwako. Nyumba ya Wajesuit".

08:42 Anapewa kitabu cha wageni na kuandika ujumbe wake. Ni heshima kubwa kwa Kanisa la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi.

08:40 Papa Francis ameingia kanisani. Anawasalimia wazee.

08:33 Papa Francis awasili mtaa wa Kangemi.

08:00 Kabla ya kwenda Kasarani, Papa Francis atazuru mtaa duni wa Kangemi na pia atembelee kanisa la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi katika mtaa huo. Papa amekuwa akitetea sana maskini na kuhimiza viongozi wahakikishe kuna usawa katika jamii.

Usalama umeimarishwa katika mtaa huo.

07:50 Wanafunzi kutoka shule mbalimbali nchini ni miongoni mwa watu waliofika asubuhi na mapema wakitaka kuingia uwanja wa Kasarani.

07:44 Papa Francis amekuwa akisisitiza umuhimu wa vijana kwa taifa. Si ajabu kwamba siku yake ya mwisho kwa Kenya, moja ya hafla ni hotuba kwa vijana. Maelfu wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wake uwanja wa michezo wa Kasarani.

07:31 Watu walianza kufika asubuhi na mapema Kasarani, na mgongamano wa magari na foleni ndefu za watu vimeshuhudiwa.

07:10 Hujambo! Leo ni siku ya tatu ya ziara ya Papa Francis nchini Kenya ambapo anatarajiwa kuzuru mtaa wa Kangemi pamoja na kanisa la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi katika mtaa huo kisha aelekee Kasarani ambako atahutubia vijana na kukutana na maaskofu wa kanisa Katoliki.