Watatu wauawa katika shambulio la kambi ya UN

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mali kambi ya vikosi vya umoja wa Mataifa

Watu 3 wamefariki katika shambulio la roketi katika kambi moja ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa kaskazini mwa Mali,Umoja wa mataifa umesema.

Wanajeshi wawili wa Umoja huo kutoka Guinea na mjenzi mmoja wameuawa katika shambulio hilo la mji wa Kidal kulingana na maafisa.

Ujumbe huo wa kulinda amani nchini Mali uliidhinishwa mwaka 2014 baada ya Ufaransa kuongoza kampeni za kijeshi kuwafurusha wapiganaji wa kiislamu kutoka eneo la Kaskazini.

Jeshi hilo kwa jina Minusma linajumlisha wanajeshi 1000 kutoka mataifa mbali mbali wengi wakiwa ni majirani wa taifa la Mali.

Wapiganaji wa kiislamu wanashukiwa kutekeleza shambulio hilo ambapo watu 14 walijeruhiwa huku watu kadhaa wakijeruhiwa vibaya.

''Kambi yetu ya Kidal ilishambuliwa mapema asubuhi na wapiganaji waliotumia makombora ya roketi'', alisema mmoja wa maafisa kutoka kwa kikosi hicho cha Minusma.