COP21: Maandamano viongozi 145 wakitua Paris

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Viongozi kutoka mataifa 145 kote duniani wanatarajiwa kuwasili Paris hii leo

Takriban viongozi 150 kutoka kote ulimwenguni wanatarajiwa kuwasili nchini Ufaransa leo tayari kwa mkutano wa dunia wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga duniani.

Mkutano huu wa kimataifa unaotarajiwa kuweka sera za kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga kwa ufupi COP21 utaanza hapo kesho.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Ufunguo wa mkutano wa COP21

Madhumuni ya mkutano huu ni kutafuta uwiano wa sera zitakazosaidia ulimwengu kupunguza ongezeko la hewa chafu ya carbon inayolaumiwa kwa ongezeko la joto duniani.

Wadadisi wanasema kuwa matuko ya kigaidi mjini Paris Ufaransa yaliyosababisha vifo vya watu 130 majuma mawili yaliyopita huenda yakatoa muamko mpya kwa wajumbe hao 40,000 kuafikiana kuhusu njia mpya ya kukabiliana dhidi ya majanga yanayotokana na mazingira iwe ni mafuriko ama njaa na ukame.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Usalama umeimarishwa vilivyo katika maeneo mengi ya Paris

Viongozi wa mataifa 147 kutoka kote duniani wamethibitisha kushiriki mkutano huo huko Paris Ufaransa.

Idadi hiyo ya viongozi inazidi 115 walihudhuria mkutano wa mwisho wa mazingira uliofanyika mjini Copenhagen mwaka wa 2009.

wakati huohuo, mamia ya maelfu ya watu wanatarajiwa kuhudhuria mikutano ya hadhara sehemu mbalimbali duniani leo Jumapili wakiunga mkono juhudi za pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga.

Kutakuwepo na zaidi ya mikutano 200,000 - ambapo mingine tayari imeanza.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Waandamanaji nchini Ujerumani

Mikutano hii imeandaliwa kufanywa siku ya kuamkia mkutano mkuu wa hali ya hewa wa umoja wa mataifa utakaofanywa Paris, Ufaransa, unaotarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa 180.

Mikutano katika miji ya Australia Bangladesh, Japan na South Africa imeshafanyika.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Viongozi wa jumuiya ya Madola, wanaokutana nchini Malta, wameunga mkono mkataba unaotarajiwa kuafikiwa Paris.

Waandamanaji hao wanashinikiza jamii za kimataifa kuhakikisha kuwa joto la dunia linapunguka na kufikia kiwango lilipokuwa kabla ya kuanza matumizi ya viwanda duniani.

Viongozi wa jumuiya ya Madola, wanaokutana nchini Malta, wameunga mkono mkataba unaotarajiwa kuafikiwa Paris.

Jumuiya hiyo ya madola yenye wanachama 53 imetoa taarifa ikieleza masikitiko yake juu ya kile inakitaja kama tishio kubwa kwa wanachama wake walio dhaifu zaidi.