Viongozi kujadili athari za joto duniani

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Wanaharakati wakiandamana Ujerumani kutaka hatua zichukuliwe kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi

Mazungumzo kuhusu Mabadiliko ya tabia nchi yanaanza rasmi asubuhi ya leo huko jijini Paris nchini ufaransa, wakuu wa nchi zaidi ya mia na hamsini wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo uliondaliwa na umoja wa mataifa.

Maandamano yamefanayika duniani kote kushinikiza kuchukuliwa hatua kupambana na ongezeko la joto duniani, jijini Paris Polisi walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwasambaratisha waandamanaji huku watu mia moja wakishikiliwa kwa kosa la kukiuka amri ya kutofanya maandamano iliyotolewa baada ya mashambulizi jijini humo.

Akifungua mkutano huo, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius, alisema ana uhakika kuwa mazungumzo hayo yatawafikisha kwenye hatua ya makubaliano chanya.

Wakati huo huo rais Obama amezuru kituo cha burudani cha Bataclan mjini Paris kutoa heshima zake kwa waathiriwa na shambulio la kigaidi wiki mbili zilizopita. Obama na rais wa nchi hiyo, Francois Hollande waliweka shada la maua kwenye ukumbi huo, ambako watu tisini waliuawa na wanamgambo wa Kiislamu waliokuwa wamejihami kwa bunduki.