Makaazi ya waliokuwa wakuu wa wizara yasakwa Kenya

Haki miliki ya picha WAIGURU TWITTER
Image caption Aliyekuwa waziri wa ugatuzi na mipango nchini Kenya, Anne Waiguru ambaye alijiuzulu wiki mbili zilizopita, baada ya kuibuka kwa madai ya ufisadi katika wizara yake

Maafisa wa tume ya kupambana na ufisadi nchini Kenya wamefanya msako katika makaazi ya waliokuwa wakuu wa wizara ya Ugatuzi na mipango .

Maafisa hao ni pamoja na aliyekuwa waziri wa ugatuzi na mipango nchini Kenya, Anne Waiguru ambaye alijiuzulu wiki mbili zilizopita, baada ya kuibuka kwa madai ya ufisadi katika wizara yake.

Msako huo ni katika harakati za uchunguzi kuhusu madai ya wizi wa dola milioni themanini kutoka wizara hiyo na tayari zaidi ya maafisa ishirini wameshtakiwa.

Huku hayo yakijiri mamia ya vijana wameandamana katika barabara za Nairobi kulalamikia ufisadi.

Vijana hawa walionekana wenye ujasiri walipokuwa wakielekea katika ikulu ya rais jijini Nairobi kuwasilisha hoja zao kwa uongozi wa nchi hii, na wengi wao wanasema kwamba ufisadi ni janga kubwa nchini na wanataka kuumaliza

Image caption Polisi walilazimika kutumia nguvu kuvunja maandamano ya vijana waliokuwa wakielekea katika ikulu ya rais jijini Nairobi kuwasilisha hoja zao kwa uongozi wa nchi hii

Kutokana na walivyokuwa, wengi wao walikuwa na hasira, Muthoni Gitau alisema "mimi ni raia aliyejawa na hamaki, nalipa Ushuru na pesa hizo zinatumiwa vibaya, tukidhani kuna mtu atakuja kutokoa, sahau, sisi wenyewe lazima tuwajibike"

Hata hivyo, kabla tu ya kufika ikulu ya Rais, walikutana na askari waliowatawanya kwa kutumia vitoa machozi kumi na moja walititiwa mbaroni na kuwachiliwa baadaye