Tanzania yachunguza ufisadi mkopo wa Stanbic

Haki miliki ya picha Tanzania Government
Image caption Tanzania imesema ndiyo iliyogundua kwanza ubadhirifu huo

Serikali ya Tanzania imesema imeanza uchunguzi wa ufisadi wa Dola milioni 6 uliohusu mkataba wa mkopo kati ya benki ya Stanbic na serikali hiyo.

Jumatatu, mahakama nchini Uingereza iliamuru kulipwa kwa fedha hizo kwa serikali ya Tanzania baada ya taasisi ya uchunguzi wa makosa makubwa ya ufisadi ya Uingereza kuwasilisha ushahidi kwamba kiasi hicho cha fedha kilipotea wakati wa uuzwaji wa hati fungani za Serikali kwa benki ya Stanbic

Katibu Mkuu Kiongozi wa Tanzania Balozi Ombeni Sefue amesema ni uchunguzi wa benki kuu ya Tanzania katika benki ya Stanbic ndio uliong’amua awali ubadhirifu huo miaka miwili iliyopita.

Amesema uchunguzi uling’amua kuwa si tu kwamba Stanbic benki nchini Tanzania iliongeza ada ya kutafuta mkopo huo kinyemelea lakini pia iligawa nyongeza hiyo kwa mtu ambaye hakuwa sehemu ya mkataba wa upatikanaji wa mkopo huo.

“Maelezo tuliyopewa ni kwamba ilibidi kuwepo na wakala wa hapa nyumbani ambaye ndiye aliyelipwa asilimia hiyo moja iliyoongezwa. Lakini benki ya Standard ilisema haikumuhitaji huyo wakala, wala sisi hapa hatukumuhitaji pia. Kwa hivyo ni utaratibu uliofanywa na benki ya Stanbic hapa Tanzania,” alisema Balozi Sefue

Aliongeza kuwa fedha hizo dola 6 milioni ziliondolewa taslimu siku chache tu baada ya kuwekwa katika akaunti

Mwandishi wa BBC Sammy Awami anasema hii ni mara ya pili kwa benki hii ya Stanbic kuhusishwa katika kashfa kubwa ya ubadhirifu wa fedha.

Mwaka jana benki hiyo ilitajwa kutumiwa kupitisha kiasi kikubwa cha pesa kilichohusiana na sakata ya Tegeta Escrow.

Balozi Sefue ameusifu uamuzi wa makamana na kuyataka mataifa makubwa kuiga mfano wa namna ya kushughulikia kesi za ufisadi zinazofanywa katika nchi zinazoendelea.