Mahakama Uturuki yaitisha uamuzi kuhusu Gollum

Gollum Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kwa mujibu wa sheria Uturuki, anayemtusi Rais anaweza kufungwa jela miaka minne

Mahakama moja nchini Uturuki imeagiza uchunguzi ufanywe kubaini sifa za mhusika mmoja katika filamu za Lord of the Rings ajulikanaye kama Gollum.

Korti imetoa uamuzi huo kwenye kesi dhidi ya Bilgin Ciftci, anayedaiwa kumtusi Rais Recep Tayyip Erdogan kwa kusambaza picha mtandaoni akimlinganisha Bw Erdogan na Gollum.

Wataalamu wanafaa kuamua iwapo ni matusi kumlinganisha Bw Erdogan na Gollum.

Haijabainika ni vipi wataamua iwapo sifa za Gollum ni mbaya au la.

Gollum ni mhusika katika filamu za The Hobbit na The Lord of the Rings za JRR Tolkien na pia katika filamu zilizoongozwa na Peter Jackson.

Alitambulishwa mara ya kwanza katika Hobbit kama “kiumbe mdogo, mchafu na mwenye ngozi telezi”. Katika Lord of the Rings, tamaa yake ya kuchukua umiliki wa pete ilimharibu mwili na akili.

Jaji aliamua wataalam waitwe baada ya kukiri kwamba hajatazama filamu zote za Lord of the Rings.

Picha zilizosambazwa na Bw Ciftci ziliwaonyesha Bw Erdogan na Gollum wakiwa wamekaa kwa njia sawa wakila, wakionyesha kushangaa na kusisimka.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari.