Marekani kutuma jeshi kushambulia IS

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri wa ulinzi wa Marekani Ash Carter

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Ash Carter amesema jeshi maalum la Marekani litatumwa kwenda nchini Iraq kupambana na wapiganaji wa Islamic State katika nchi za Iraq na Syria.

Amesema majeshi hayo yatafanya operesheni hiyo ikiwa ni pamoja kuwaokoa mateka na kuwakamata viongozi wa I S.

Wakati huo huo Rais wa Syria Bashar Al Assad amesema uamuzi wa Urusi kuingia vitani katika nchi yake kumedhoofisha nguvu ya wapigani wa Islamic state tofauti na majeshi ya Marekani ambayo yamefanya kundi hilo kujiimarisha zaidi.

Waziri huyo wa ulinzi wa Marekani Ash Carter alitoa kauli hiyo wakati akiongea kwenye Kamati ya Congress huko Washtong nchini Marekani.

"Kuongeza kasi hiyo tutatuma tena kwa amri ya rais Obama na kwa ushauri wa mwenyekiti na wangu, Kikosi maalum cha kijeshi nchini Syria kusaidia kupambana na wapiganaji wa ISIL. Majeshi hayo maalum ya uwezo maalum wa kufanya kazi mbali mbali. Litatusaisia kufanya upelelezi wa ardhini kusaidia majeshi ya nchi hizo na watarudisha maeneo yaliyochutekwa na ISIL. Mahali tutakapopata nafasi kuteka maeneo tutapanua harakati zaidi."

Aidha Cater amesema katika maeneo ya Iraq majeshi hayo yatapambana na vilivyo na wapiganaji wa Islamic State.

"Kwa uratibu kamili na serikali ya Iraq tutapeleka majeshi maalum kupambana kwa kusaidia majeshi ya Iraq na wapiganaji wa Peshmega kuzidi kuwashughulikia ISIL. Majeshi haya maalum kwa muda wote watakuwa na uweza wa kuendesha opesheni kuwaachia huru mateka kukusanya taarifa za kiusalama na kuwakamata viongozi wa ISIL."

Wakati huo huo Rais wa Syria Bashar Al Assad amesema uamuzi wa Urusi kuingia vitani katika nchi yake imebadilisha hali katika uwanja wa vita. Katika mahojiano kwenye kituo cha televisheni cha Czech Assad amesema tangu Urusi ilipoingilia kati kijeshi wapigani wa Islamic State na makundi mengine ya jihad yamedhoofika, na amesema anaamini msaada wa Urusi utaendelea. Amesema majeshi ya Urusi yamekuwa na uwezo na uamuzi wa hali ya juu tofauti na majeshi ya ushirika yanayoongozwa na Marekani.

Katika hatua nyingine naye Waziri Mkuu wa Uingereza amewaomba wabunge wa chama cha Conservative kuunga mkono mpango wake wa majeshi ya Uingereza kufanya mashambulizi ya angani dhidi ya Islamic State nchini Syria.