Australia yasema ina matumaini MH370 itapatikana

Australia Haki miliki ya picha AP
Image caption Australia imesaka ndege hiyo eneo la kilomita 75,000 mraba kufikia sasa

Maafisa nchini Australia wamesema wanaamini wanasaka mabaki ya ndege ya shirika la Malaysia Airlines nambari MH370 iliyotoweka mwaka jana pahali sahihi.

Utathmini mpya wa takwimu uliofanywa na idara ya usalama unaonyesha uwezekano mkubwa ndege hiyo imo maeneo ya kusini katika Bahari ya Hindi, ambako sasa juhudi zaidi zitaelekezwa.

MH370 ilikuwa safarini kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing ilipotoweka Machi 2014 ikiwa na abiria 239.

Naibu Waziri Mkuu Warren Truss alisema maafisa wana “matumaini” kwamba itapatikana.

Lakini alisema operesheni hiyo huenda isikamilike kabla ya Juni 2016.

Haki miliki ya picha Reuters

Kipande cha ubawa wa ndege, kijulikanacho kama flaperon, kilipatikana visiwa vya Reunion Julai, takriban kilomita 4,000 kutoka eneo ambalo ndege hiyo imekuwa ikitafutwa.

Ingawa uchunguzi Ufaransa ulionyesha kilitoka kwa MH370, maafisa wanasema kilifikishwa huko na mawimbi ya baharini na hilo halijaathiri juhudi za kutafuta mabaki ya ndege hiyo.