Mji ulioachwa mikononi mwa wanawake Burkina Faso

Marafiki
Image caption Nematou na Alimata wamekuwa marafiki wa kufa kuzikana

Kuna mji Afrika Magharibi ambako ni kawaida kwa wanaume kuondoka na kwenda kutafuta ajira Italia. Wanawake huachwa nyuma na waume zao kwa miaka mingi, hata miongo. Lakini mji wa Beguedo nchini Burkina Faso si mji wa kipekee. Kuna miji mingi sana Afrika ambako jambo hili hufanyika, wanaume husafiri kwenda nchi jirani au Ulaya wakitafuta kazi.

Jamii huishi vipi wanaume wanapoishi maelfu ya maili mbali na nyumbani? Mwandishi wa BBC alitembelea mji huo na kukutana na wanawake walioachwa nyumbani na waume walioenda kutafuta ajira.

Alimata Bara daima hujaa tabasamu, akiwa na ucheshi. Leo anacheka masaibu yaliyomkumba – kama “mke mseja”. Miaka saba iliyopita, akiwa na umri wa miaka 17, aliolewa na “Mwitaliano”, ambalo ni jina la utani wanalopewa wanaume walioenda kufanya kazi Italia.

“Tulikutana sokoni, na tukaanza kuzungumza,” anakumbuka. "Kisha alileta kokwa za kola kwa wazazi wangu. Baada ya siku 10 tukaoana.”

Zamani za kale, ilichukua miezi kadha kupanga harusi eneo la mashambani kama hapa. Mtafuta uchumba alihitaji kufanya kazi katika shamba la mzazi wa msichana, kuaminika, na kuonyesha kwamba anaweza kukidhi mahitaji na kuwa mume mzuri kwa mwanamke aliyemtamani.

Lakini sasa, miezi imegeuka kuwa wiki – na wakati mwingine siku, pale mume mtarajiwa huwa likizoni na anapanga kurejea Ulaya.

Tangu kuolewa, Alimata amekaa chini ya miezi sita pamoja na mumewe. Ana binti kwa jina Omayma, mwenye umri wa miaka sita sasa. Mtoto wao wa pili, Obaidou mwenye umri wa miaka mitatu, amemuona babake mara moja pekee.

Mjini Beguedo, kilomita 230 (maili 140) kusini mashariki mwa mji mkuu, Ougadougou, wanawake wengi wanapitia masaibu sawa na ya Alimata. Nematou, anayeishi karibu sana na Alimata, ameolewa na kakake Saada, ambaye pia anafanya kazi ng’ambo.

Image caption Nematou hujifanyia kazi nyingi

Nematou na Alimata wanakaribiana sana kwa umri, na wawili hao sasa wamekuwa marafiki wa kufa kuzikana, wakisaidiana katika kuwalea watoto wao, na kufanyiana mzaha kuhusu maisha yao.

Nusu ya akina mama wote katika kijiji hicho wamo katika hali sawa, kwa mujibu wa meya wa zamani Beatrice Bara.

Ndiyo matokeo ya maelfu ya wanaume kutoka Afrika kuhamia Ulaya kutafuta kazi.

Wanapooa, wanaume hawa huahidi kurejea nyumbani mara kwa mara, au kuja kuwachukua wake zao wakishatulia huko ugenini. Baadhi wamefanya hivyo. Lakini hiyo ilikuwa kabla ya mgogoro wa kiuchumi kuzuka, na kabla ya Ulaya kugeuzwa kuwa ngome ambayo wahamiaji wanazuiwa kuingia.

Alimata alipoolewa na Saada mwaka 2008, alidhani kwamba muda mfupi baadaye angejiunga naye Italia. “Alidhani angenichukua niende naye, lakini baadaye alipoteza kazi,” anasema.

Image caption Alimata amefungua biashara ndogo ya kuuza makaa kujikimu kimaisha

Hata hivyo, ingawa Saada aliweza kujengea Alimata nyumba nzuri yenye chumba kimoja cha kulala nyumbani kwao, hajafanikiwa vya kutosha Italia kuweza kutuma pesa nyingi nyumbani, huwa anatuma franka 25,000 CFA (takriban £25) hapa na pale, baada ya miezi kadha.

Kwa bahati, hajakuwa akitegemea pesa za Saada pekee. Alianzisha biashara ndogo ya kuuza makaa. Pia hua anauza sehemu ya mavuno kutoka shambani, na hivi ndivyo anavyoweza kujimudu kimaisha.

Waume kutoweka

Katika baadhi ya barabara za mji huo wa Beguedo, nyumba zenye paa za makuti zinapakana na nyumba kubwa.

Nyumba hizi kubwa sana ni za Waitaliano “wakongwe”, wale waliohamia Ulaya kabla ya mgogoro wa kiuchumi, na walipata kazi nzuri ukilinganisha na Waitaliano “wapya” ambao walifuata baadaye.

Mumewe Mominata Sambara alielekea Italia karibu miaka 30 iliyopita, na alirejea nyumbani mara nyingi kiasi cha kuweza kujaliwa watoto saba.

“Mambo yalienda vyema. Kila mwezi, angetuma franka 50,000 za CFA (karibu £50). Alitujengea nyumba,” anasema, akiwa ameketi juu ya mkeka maridadi nje ya nyumba yake, ambayo ina veranda kubwa, mtambo wa mawasiliano ya simu na hata setilaiti ya kunasa mawimbi ya runinga.

“Lakini mambo sasa ni tofauti,” anasema.

Wanaume vijana mjini Beguedo bado wanaamini maisha ni mazuri Italia licha ya hayo yote, labda kwa sababu wanaorejea hujionyesha na kuficha matatizo waliyokumbana nayo.

“Watu walioondoka lakini hawakuweza kutengeneza pesa huko ng’ambo hurudi wamefadhaika, na kawaida huwa hawarudi kuishi katika vijiji vyao,” anasema Prof Mahamadou Zongo, mwanasosiolojia katika chuo kikuu cha Ouagadougou.

“Huenda kuishi mjini ambako hawawezi kutambulika kwa urahisi.”

Ndoto ya kwenda Italia imeathiri hata idadi ya wale wanaoenda shuleni Beguedo. Wanaume vijana hupoteza hamu ya kwenda shuleni kwa sababu huonelea heri wakatengeneze kile wanachoona kama pesa rahisi Italia, huku wanawake vijana nao wakishawishika kuacha shule na kuoa Waitaliano.

Image caption Wanaume wanaoshindwa kufanikiwa ugenini huamua kukaa mijini wanaporejea nyumbani

Lakini Zongo anasema baadhi ya wanawake sasa wanafahamu matatizo haya.

“Kati ya siku ya harusi na siku ya pili mwanamume kurejea kijijini, inaweza kupita hadi miaka mitano, sita, au saba,” anasema.

“Wakati huo, mke huishi na mashemeji wake. Lazima awe mtiifu na mpole. Anafuatiliwa kwa karibu. Anaweza kukataliwa kwa jambo ndogo.”

Na pia kuna hatari ya kulazimika kumkubali wa pili, kama Adiassa (si jina lake halisi), mwenye umri wa miaka 50, anavyosimulia.

Mumewe wa miaka 30 alikaa Italia kwa miongo miwili, na hata akawachukua wana wao wawili wa kiume wakaishi huko na kufanya kazi.

“Mwanzoni, mambo yalikuwa mazuri, angerudi baada ya miaka kadha, na kutuma pesa nzuri,” anakumbuka.

"Naam, mambo yalikuwa mazuri sana wakati huo,” anasema, huku akicheka na kutoa sauti sawa na ya busu.

Lakini miaka sita iliyopita, mume wangu alinijulisha kwamba alipanga kuoa mke wa pili. “Nilikataa hilo. Hakuna mwanamke anayependa mumewe aoe mke wa pili, lakini hakunipa nafasi.”

Wanaume kuoa wake wengi

Watu wa kabila la Bissa wanaoishi Beguedo na maeneo ya karibu Burkina Faso ni Waislamu. Inaruhusiwa mwanamume kuoa wake wengi. Hata hivyo lilikuwa pigo kubwa kwa Adiassa kwani sio tu kwamba mumewe alioa mwanamke mchanga bali pia alimchukua na akaenda kuishi naye Ulaya.

Mumewe huwa hamtumii pesa tena, au hata kumpigia simu. Sasa huwa anategemea watoto wake.

Awa Sagne amepitia hali sawa.

Miaka mitatu iliyopita, kuashiria ufanisi wake Italia, mumewe alimuoa mke mwingine. Baada ya miaka mingi ya kuhangaika kujikimu kimaisha, Awa, aliye na umri wa miaka 38 sasa, anaishi na mke mwenza ambaye ni mdogo wake wa umri kwa karibu miaka 20.

Image caption Huduma ya Western Union ni moja ya njia zinazotumiwa kutuma pesa kutoka nje ya Burkina Faso

Ni rahisi sana kugundua pigo alilopata Awa anaposimulia kuhusu kisa kimoja miaka mingi iliyopita, mumewe alipomtumia kiasi kidogo sana cha pesa.

“Wakati mmoja alinitumia franka 2,500 pekee! [karibu £2] Nitafanya nini na pesa kama hizo? Niliangalia tena bahasha, sikuamini, nilimrudishia.”

Baadaye alimpigia simu. “Asante lakini sitazipokea,” alimwambia. “Heri nijifanyie kazi na kupata pesa hizo kwa jasho langu.”

Ni kama kujikinga dhidi ya hawa kwamba Malika (si jina lake), mwenye umri wa miaka 22, alifungua akaunti ya benki kisiri baada ya kuolewa na Mwitaliano miaka mitatu iliyopita.

Kila anapoweza, huwa anatenga kiasi kidogo cha pesa, hata kama ni shilingi kadha tu.

“Huwezi ukamwambia mumeo kila kitu. Na huwezi ukamwamini 100%,” anasema.

Hata kama anamtumia pesa za kutosha mahitaji yaje, bado yeye atafanya kazi, anasema.

Methali moja Bissa inaeleza msimamo wake: “Ukilalia mkeka wa mtu mwengine, ni bora tu ulalie sakafu.”