Raia Nigeria walalamikia ‘sheria ya mtandao’

Mtandao Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wengi wanasema sheria hiyo itaathiri wanaotumia mitandao ya kijamii

Raia wa Nigeria wamekuwa wakilalamika katika mitandao ya kijamii kupinga mswada wa sheria mpya ambao wanasema lengo lake ni kunyima watu uhuru wa kujieleza.

Mswada huo ambao unajadiliwa katika Bunge la Seneti unalenga kuzuia “malalamiko ambayo hayana msingi”.

Kwenye Twitter, raia hao wamekuwa wakitumia kitambulisha mada #NoToSocialMediaBill kupinga mswada huo ambao unapendekeza adhabu ya kufungwa hadi miaka saba jela au faini ya $25,000 (£16,000) kwa yeyote anayeeneza habari za uongo.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeshutumu sheria hiyo na kusema ni juhudi za kunyima watu uhuru wa kujieleza.

Mamilioni ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii, pamoja na wale wanaotuma arafa, wanaweza wakaatihiriwa na mswada huo iwapo utapitishwa na kufanywa kuwa sheria, shirika hilo limesema kupitia taarifa.

Seneta Bala Ibn Na'allah wa chama tawala cha All Progressive Congress, hata hivyo amewajibu wanaosema mswada huo unalenga kunyima watu uhuru wa kujieleza, akisema lengo ni kuzuia kuenea kwa “habari za uongo”.

"Huwezi ukaandika habari za uongo kwa sababu ni mtandao wa kijamii,” aliambia BBC Hausa.

Mwandishi wa BBC mjini Abuja Nasidi Adamu Yahya anasema mishahara mikubwa ya wabunge Nigeria ni moja ya mambo ambayo yamekuwa yakiangaziwa sana kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.