Waliokwepa kulipa kodi bandarini Tanzania wagunduliwa

TRA
Image caption Maafisa wa mamlaka ya mapato wametakiwa kutangaza utajiri wao

Kampuni 43 ambazo zinamiliki makontena 329 yaliyokamatwa bandarini Tanzania wakati wa ziara ya kushtukiza ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa zimetambuliwa.

Wasimamizi wa kampuni hizo wamepewa nafuu ya siku saba na Rais John Magufuli kulipa kodi inayohitajika bila adhabu.

Kaimu kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) Dkt Philip Mpango amesema sasa zimesalia siku sita kwa kampuni hizo kulipa kodi inayotakikana.

Kampuni 4 tayari zimejitokeza na kulipa Sh5 bilioni.

Makonteina hayo yalikamatwa katika bandari kavu ya kampuni ya Said Salim Bakhresa.

Bidhaa zilizokuwemo ndani ya makontena hayo ni pamoja na matairi ya magari,vifaa vya ujenzi, betri za magari, nguo na bidhaa nyingine.

Watuhumiwa 8 wanaoshukiwa kuhusika katika kupitishwa kwa makontena hayo 329 wamefikishwa Mahakama ya Kisutu leo wakikabiliwa na makosa ya kuhujumu uchumi, kusababisha hasara ya Sh12.7bn.

Aidha, kufikia sasa, watumishi 35 wa TRA katika ngazi mbali mbali wamesimamishwa kazi wakiwemo 27 waliokamatwa katika ziara hiyo ya kushtukiza ya Bw Majaliwa.

Wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano huku uchunguzi ukiendelea.

Hayo yakijiri, watumishi wote wa TRA wametakiwa kuwasilisha taarifa sahihi ya orodha ya mali zao zote kwa ajili ya uhakiki wa kina kufikia tarehe 15 Desemba.