Aliyekataa tiba akisema amepoteza mng’ao afariki

Matibabu Haki miliki ya picha Thinkstock
Image caption Jaji aliamua mwanamke huyo hawezi kushurutishwa kupokea matibabu

Mwanamke aliyekataa matibabu ya figo kuokoa maisha yake nchini Uingereza, akisema ameshapoteza mng’ao, amefariki.

Mwanamke huyo wa umri wa miaka 50 aliyetambuliwa tu kama C, aligonga vichwa vya habari baada ya jaji kuamua kwamba ana haki ya kukataa kupokea matibabu ya kusafisha damu.

Figo za C ziliharibika baada yake kunywa dawa kupita kiasi akitaka kujiua.

Mahakama iliambia kwamba katika maisha yake, C aliangazia zaidi "sura yake, wanaume na vitu vya thamani.”

Mmoja wa bindi zake aliambia mahakama: “Kupona kwake si kwamba figo zake zianze kufanya kazi tena pekee, bali atahitaji kupata ‘mng’ao’, jambo ambalo anaamini hawezi kuapata tena kutokana na umri wake.”

Mwaka uliopita, C alikuwa amepatikana na saratani ya matiti lakini akakataa matibabu akisema matibabu hayo yangemfanya kuwa mnene.

Baada ya kupata matatizo ya figo, wakfu wa Huduma ya Taifa ya Afya Uingereza katika hospitali ya King’s College ulitaka alazimishwe kupokea matibabu.

Lakini Jaji MacDonald, kwenye uamuzi alioutoa Novemba 13, alisema C ana uhuru wa kufanya uamuzi.