Waafrika walio orodha ya Wanawake 100 wa BBC

Kwa mwaka wa tatu sasa, BBC imetayarisha orodha ya ‘Wanawake 100’ ambao wanawapa motisha wanawake wengine kwenye kazi zao na katika shughuli zao za kawaida.

Katika orodha ya Wanawake 100 wa mwaka huu, hawa ndio waliojumuishwa kutoka Afrika:

1. Alimata Bara

Miaka: 24

Taifa: Burkina Faso

Alimata anatoka Beguedo, mji ulioko mashariki Burkina Faso, na mumewe alihamia Italia kutafuta kazi. Tangu kuoana kwao mwaka wa 2009, mumewe amerudi nyumbani mara mbili.

Alifikiria kuolewa na mhamiaji kungemuwezesha kuepukana na hali ngumi za mashambani, na angeenda naye Ulaya. Lakini bado yaligeuka kinyume, na amebaki kuwalea watoto wake wawili.

2. Sana Ben Ashour

Miaka: 60

Kazi: Mwanaharakati wa kiraia

Taifa: Tunisia

Sana alianzisha kituo cha kutunza wanawake kwa jina BEITY (neno la Kiarabu linalomaanisha Nyumbani kwangu) mwaka 2012. Alitiwa motisha na mahitaji ya haki na usawa kwa wanawake katika jamii yake.

Ni kituo cha kipekee huko Tunisia ambacho husaidia wanawake ambao hawajaolewa pamoja na wanawake wengine wanaohitaji msaada, kama vile walioathirika na umaskini na mizozo ya kinyumbani.

3. Fatou Bensouda

Miaka: 54

Kazi: Mwendeshaji mashtaka ICC

Taifa: Gambia

Haki miliki ya picha AFP

Mwendeshaji mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC huko Hague, ni mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kushikilia mkuu katika mahakama ya ICC

Amewahi kuwa mtumishi wa umma kwenye serikali ya Gambia, na amezawadiwa tuzo nyingi kwa mchango wake katika sheria za jinai.

4. Naomi Bya’Ombe

Miaka: 15

Kazi: Mwanafunzi

Taifa: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Naomi anaishi Kinshasa, DRC na anapenda kuimba na kucheza.

Naomi ni mtoto wa tano katika familia ya watoto saba na anaishi na binamu zake wawili. Kwa sasa anakaribia kumaliza shule ya upili na huimba kwaya kanisani kila Jumapili.

Naomi ameangaziwa kwenye filamu yetu ya ‘msichana mzuri’.

5. Eveles Chimala

Miaka: 29

Mazi : Mkunga

Taifa: Malawi

Baada ya kufanya kazi katika hospitali iliyokuwa na kazi nyingi Malawi, Eveles aliamua kurudia masomo yake ili kusaidia nchi yake kukabiliana na idadi ya vifo vya wajawazito.

Yeye hufuatilia partograph – kifaa kilichoundwa kuwasaidia wakunga kufuatilia kina mama wanapojifungua.

6. Nkoszana Dlamini-Zuma

Miaka: 66

Kazi: Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika

Taifa: Afrika Kusini

Daktari wa afya aliyehitimu, Nkoszana ni Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika iliyoko Addis Ababa, Ethiopia.

Hapo mwanzo alikuwa mwanaharakati wa ANC na alikaa miaka kadha uhamishoni wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi. Alijitosa katika siasa, na kujiunga na AU mwaka 2012. Ndiye mwanamke wa kwanza kuongoza tume hiyo.

7. Isabel dos Santos

Miaka : 42

Kazi: Mwekezaji

Taifa: Angola

Isabel dos Santos ni mwekezaji na kwa mujibu wa jarida la Marekani la Forbes, ndiye mwanamke tajiri Afrika. Ni binti wa kwanza rais wa Angola, Jose Eduardo dos Santos na amewekeza kwa mafuta na gesi, benki, mawasiliano na kampuni za vyombo vya habari.

7. Ernestina Edem Appiah

Miaka: 38

Kazi : Mfanyibiashara wa kijamii

Taifa: Ghana

Ernestina (Tina) ni mwazilishi wa klabu ya Ghana Code Club, shirika ambalo huwapa watoto wa Ghana walio na umri wa miaka 8 hadi 14 ujuzi wa kuandika programu za kompyuta.

Anataka kuzindua Ghana Code Club, katika shule zote za kawaida Ghana, ikiwezekana.

9. Aissa Edon

Miaka: 33

Kazi: Mkunga

Taifa: Ufaransa

Aissa ni mkunga ambaye ana utaalamu katika kuangazia matatizo ya ukeketaji wa wanawake.

Ni mzaliwa wa Mali na amelelewa ufaransa. Mwenyewe alikeketwa alipokuwa mtoto. Kwa hivi sasa anafanya kazi London akiwasaidia wanawake ambao hupata shida wakati wa ujauzito na kuzaa kutokana na ukeketaji.

10. Nawal el-Sadaawi

Miaka: 85

Kazi: Mwandishi wa vitabu

Taifa: Mmisri

Mwaandishi maarufu, ameandika zaidi ya vitabu 40 na hupenda kupigania haki za wanawake katika mji wake. Witabu vyake wamekuwa na ushawishi mkubwa sana kwa wanawake wa Misri.

Kitabu chake cha kupigania jinsia na wanawake, kilichopigwa marufuku nchini Misri miongo miwili iliyopita, kilifafanua kuhusu jinsia na ukeketaji

11. Misraa Jimaa

Kazi: Mfanyakazi wa afya ugani

Taifa: Ethiopia

Misraa amefunzwa kwa mwaka mmoja huduma za afya na kwa hivi sasa anahudumu katika eneo moja nchini humo.

Husaidia kuwafundisha wananchi kuhusu masuala ya afya, upangaji uzazi, chanjo na lishe bora na hufanya kazi na wanawake na watoto wadogo.

Misraa ameangaziwa katika makala ya wahudumu wa afya ulimwenguni

12. Linda Kwamboka

Miaka: 27

Kazi : Mfanyibiashara

Taifa: Mkenya

Linda ni mwazilishi wa kampuni ya Mfarm ambayo huwawezesha wakulima nchini Kenya na ulimwengu mzima.

Kampuni yake huwapatia wakulima vifaa ambavyo vinaweza kuwajulisha wakulima kuhusu hali ya soko, wakulima wastani wanachohitaji na kuwaunganisha na wengine ili wauze mazao yao kwa pamoja.

13. Luteni Kamanda Zimasa Mabela

Umri: 38

Kazi: Kapteni katika jeshi la wanamaji

Taifa: Afrika Kusini

Zimasa alilelewa katika kijiji cha mashariki mwa Afrika Kusini na hakuwahi kuona bahari hadi alipotimu umri wa miaka 18.

Alipata motisha kutoka kwa mazungumzo na wanajeshi alipokuwa chuo kikuu, aliwasilisha ombi la kazi la kwanza kama afisa wa kusimamia vipindi vha redio mwaka 1999. Kwa hivi sasa anaishi katika mji wa Cape Town.

14. Emi Mahmoud

Umri: 22

Kazi: Mshairi

Taifa: Sudan na Marekani

Emi Mahmoud ni mshairi na mwanaharakati kutoka Darfur na kwa sasa anashikilia taji la World Poetry Slam Champion wa mwaka 2015.

Emi yumo kwenye mwaka wake wa mwisho Chuo Kikuu cha Yale akisomea antholojia na biolojia ya molekuli.

Lengo lake kuu ni kupunguza pengo katika huduma za afya ya uzazi na afya ya watoto na kuwezesha wanawake kupitia ushairi na uhuru wa kujieleza.

15. Catherine Mahugu

Umri: 27

Kazi: Mjasiriamali

Taifa: Mkenya

Mwanzilishi wa Soko, ukumbi wa kufanya biashara dijitali ambao huwawezesha mafundi na wasanii kuuza bidhaa na vito moja kwa moja hadi kwa wateja.

Lengo lake ni kuzidisha biashara ya moja kwa moja kati ya watengenezaji bidhaa Afrika na wateja kote duniani.

15. Nemata Majeks-Walker

Umri: 68

Kazi: Mwanaharakati

Taifa: Sierra Leone

Mwaka 2001, Nemata alianzisha kundi la 50/50 nchini Sierra Leone ambayo huwahimiza na kuwawezesha wanawake kushiriki katika siasa nchini humo.

Kundi hilo liliibuka la kwanza kushinda tuzo kuu ya Madeleine Albright mwaka 2007.

16. Karabo Mathang

Umri: 28

Kazi: Mjasiriamali

Taifa: Afrika Kusini

Karabo ndiye wakala wa kwanza Afrika Kusini kuidhinishwa na Fifa.

Alianzisha P Management kutafuta wachezaji wenye vipaji na kuwasaidia kupata mikataba na klabu mbalimbali.

17. Verashni Pillay

Umri: 31

Kazi: Mhariri wa gazeti

Taifa: Afrika Kusini

Verashni ndiye mhariri mkuu wa Mail & Guardian, gazeti huru la uchunguzi Afrika Kusini.

Alishinda pia tuzo za CNN African Journalism Award, a Standard Bank Sikuvile Award na Open Society Foundation journalism fellowship.

18. Claire Reid

Umri: 29

Kazi: Mjasiriamali

Taifa: Afrika Kusini

Claire aliunda Reel Gardening katika juhudi za kurahisisha kazi shambani.

Kampuni yake hutengeneza vifaa ambavyo huingiza mbegu ardhini katika kina kinachohitajika na kwa upana ufaao na hivyo kazi inayosalia ni kupanda tu na kunyunyizia maji.

19. Rabia Salihu Said

Umri: 52

Kazi: Mwanafizikia

Taifa: Nigeria

Rabia ni mwanafizikia ambaye ameshiriki katika miradi ya kitaifa na ya mashinani inayohimiza vijana kujiunga na fani ya sayansi. Amefanya hivi kwa miaka 30.

Mwanamke huyu mwenye watoto sita, alipokea tuzo ya Elsevier 2015 kwa juhudi zake katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuharibiwa kwa misitu.

20. Amina Sboui

Umri: 21

Kazi: Mwandishi na mwanaharakati

Taifa: Tunisia

Amina aligonga vichwa vya habari 2013 kwa kupakia kwenye Facebook picha yake akiwa kifua wazi akiwa ameandika “mwili wangu ni wangu na si kiini cha heshima kwa mtu yeyote” kifuani.

Baada ya kuachiliwa kutoka jela, Amina alienda Paris kwa masomo. Amerejea Tunisia majuzi na huhariri na kuchapisha gazeti linaloangazia masuala ya wanawake.

21. Alek Wek

Umri: 28

Kazi: Mwanamitindo/Balozi wa UN

Taifa: Sudan

Mmoja wa wanamitindo wanaotambuliwa sana duniani, Alek alikulia Sudan wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kabla ya familia yake kutafuta hifadhi Uingereza miaka ya 1990.

Alijiingiza katika uanamitindo na akafanikiwa sana. Kama balozi wa uhusiano mwema wa UN, yeye huzuru kambi za wakimbizi Sudan Kusini mara kwa mara.

22. Marie-Ange Zimndou Koutou

Umri: 42

Kazi: Msaidizi wa muuguzi

Taifa: Jamhuri ya Afrika ya Kati

Huwezi kusikiliza tena

Marie-Ange amekuwa akifanya kazi katika idara ya the kutunza watoto katika hospitali inayosimamiwa na Medecins Sans Frontieres eneo la mashambani la Kabo kwa miaka tisa iliyopita.

Wahudumu wa afya ni wachache mno CAR, na licha ya kupokea mafunzo miezi mitatu pekee, Marie-Ange hufanya kazi inayofanywa na wauguzi waliohitimu maeneo mengine duniani.