Iraq yaitaka Uturuki iondoe majeshi Mosul

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wanajeshi wa Uturuki waliingia eneo hilo kuwapa mafunzo wapiganaji wa Kikurdi

Serikali ya Iraq imeiamuru Uturuki iondoe wanajeshi wake katika eneo la mpakani karibu na mji wa Mosul ambalo linadhibitiwa na wapiganaji wa Islamic State.

Afisi ya Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi imetaja hatua ya Uturuki kuingiza majeshi maeneo ya Uturuki kuwa kuingilia uhuru na mipaka ya taifa hilo.

Mamia ya wanajeshi wa Uturuki, wakitumia vifaru, walivuka mpaka na kuingia eneo hilo, lengo lao likiripotiwa kuwa kuwapa mafunzo wapiganaji wa Kikurdi nchini Iraq ambao wamekuwa wakipambana na wapiganaji wa Islamic State.

Ripoti zinasema wanajeshi 150 walikuwa wametumwa katika mji wa Bashiqa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wapiganaji wa Islamic State waliteka mji wa Mosul mwaka jana

Taarifa ya afisi ya Bw al-Abadi imeitaka Uturuki kuheshimu ujirani mwema na kuondoa wanajeshi eneo hilo lililo kaskazini mwa Iraq.

Mji wa Mosul umekuwa ukidhibitiwa na wapiganaji wa Islamic State tangu mwaka jana na juhudi za Iraq kujaribu kuukomboa hazijafanikiwa.