Maelfu waandamana kupinga mabadiliko Korea Kusini

Waandamanaji Haki miliki ya picha AP
Image caption Waandamanaji wanasema mpango wa serikali utaathiri demokrasia nchini humo

Maelfu ya watu wameandamana leo nchini Korea Kusini kupinga mipango ya serikali ambayo wanasema itadhoofisha demokrasia.

Ingawa watu wengi walijitokeza kwa maandamano hayo, hakukutokea vurugu.

Maafisa wa polisi takriban 18,000 walitumwa mji mkuu Seoul kuwadhibiti waandamanaji.

Waandamanaji wanapinga mipango ambayo inajumuisha mabadiliko katika sheria za leba na udhibiti zaidi katika vitabu vya historia.

Wanasema hatua hiyo itafuta maovu yaliyotendwa na viongozi wa kiimla wa zamani Korea Kusini.

Haki miliki ya picha AP

Waandamanaji pia wamekasirishwa na hatua ya serikali hafidhina ya Rais Park Geun-hye ya kupitisha mpango wa kuwafuta kazi wafanyakazi kwa kutegemea utendakazi wao.

Kadhalika, mpango wa kuweka kiwango kwenye mishahara ya maafisa wakuu ili kuwafanya waajiri kuwapa kazi vijana na kupunguza ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

Waandamanaji 14,000 walijitokeza, ambao ni wachache ukilinganisha na zaidi ya 60,000 waliojitokeza maandamano ya Novemba 14.