Upinzani washinda uchaguzi Venezuela

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bendera ya muungano wa upinzani wakipeperusha bendera kwa furaha.

Tume ya uchaguzi nchini Venezuela imethibitisha kwamba muungano wa upinzani umeshinda wabunge tisini na tisa kati ya mia moja na sitini na saba katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa juma lililopita kwa mbili ya tatu ya kura zote zilizopigwa.

Ushindi huo wa kishindo unaupa muungano wa kidemokrasia nguvu za kutosha kukabiliana na rais mwenye mrengo wa kijamaa, Nicolas Maduro.

Hili linajumuisha uwezo wa kubadili uteuzi wa nafasi za majaji wa mahakama kuu nchini humo na hata ikibidi kuanzisha kura ya maoni endapo watahitaji kufuta mamlaka ya Bw Maduro .

Muungano huo wa kidemokrasia nchini Venezuela umesema kwamba vipaumbele vyake pindi watakapoanza majukumu ya kuwatumikia raia wa nchi hiyo ni kuwaachilia huru viongozi wote wa upinzani walioko jela, na kuunusuru uchumi wa nchi hiyo ambao unakwenda kombo.

Ushindi huo kwa upande wa upinzani unahitimisha utawala wa miaka kumi na saba uliokuwa una hodhiwa na chama cha kijamii cha marehemu Rais Hugo Chavez.