Bozize azuiwa kuwania urais CAR

Bozize Haki miliki ya picha
Image caption Bozize aliondolewa madarakani 2013

Mahakama ya kikatiba nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati imemzuia Rais wa zamani François Bozizé kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mahakama hiyo imechapisha orodha ya wagombea 30 wanaoruhusiwa kuwania kwenye uchaguzi huo wa Desemba 27, na jina la Bw Bozizé halimo.

Watu 14 waliokuwa wamewasilisha maombi ya kutaka kuwania wamekataliwa.

Bw Bozizé aliongoza taifa hilo kabla ya kufurushwa na wapiganaji wa Seleka na kwa sasa anaishi uhamishoni.

Ameapa kuendelea kupigania watu wa CAR.

"Tumefahamishwa sasa hivi kuhusu uamuzi huo, ambao ni wa aibu sana na umetolewa kwa shinikizo kutoka kwa mataifa ya nje,” alisema.

"Unaona sasa Bozizé, aliyeongoza kwa miaka mingi sasa ni mgeni nchini mwake...Hata hivyo tutaendelea kupambana, hili litaendelezwa na watu wa CAR, ili mapenzi ya watu wa Afrika ya Kati yatimie.”