Rais wa Argentina kupambana na rushwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais mpya wa Argentina Mauricio Macri

Rais mpya wa Argentine, Mauricio Macri, katika hotuba yake ya kwanza ameahidi kupambana na rushwa na kueleza wazi kuwa hatakuwa na huruma kwa mtu yeyote atakaye kwenda kinyume na sheria za nchi hiyo bila kujali uhusiano wao wa kisiasa.

Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kula kiapo cha urais, Bwana Macri aliongeza kusema kwamba amepokea madaraka huku akijua kuwa amerithi changamoto changamoto nyingi, na kusema kwamba kwa yeye, siasa ni kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya watu.

Wakati hayo yakijiri Rais aliyeondoka madarakani, Cristina Fernandez de Kirchner, alisusia kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais Mauricio Macri, kwa sababu ya mzozo juu ya itifaki.

Hata hivyo maelfu ya raia wa nchi hiyo walijipanga katika mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo, Buenos Aires, ili kumshangilia rais mpya,huku wakipepea bendera za nchi hiyo zenye rangi za buluu na nyeupe.

Ushindi wa rais Macri ulipatikana baada ya kurudiwa kwa uchaguzi ambao ulifanyika mwezi uliopita na kuhitimisha utawala wa miaka kumi na miwili wa serikali yenye mrengo wa kushoto uliokuwa chini ya utawala wa rais mstaafu Fernandez na marehemu mumewe Nestor Kirchner.