Jeshi la Nigeria lawaokoa watu 200

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Jeshi la Nigeria

Jeshi la Nigeria limesema kuwa limewaokoa zaidi ya watu 200 ambao walikuwa mateka wa kundi la wapiganaji wa Boko Haram.

Vikosi vya usalama vilikivamia kijiji kimoja kinachodhibitiwa na kundi hilo kaskazini mashariki mwa jimbo la Yobe.

Wanawake, watoto na wazee ni miongoni mwa watu waliookolewa na jeshi la Nigeria. Walitekwa nyara na wapiganaji wa Boko Haram kutoka vijiji tofauti na wamekua wakitumiwa kama ngao.

Msemaji wa jeshi amesema wapiganaji watano waliuawa na silaha kadhaa kupatikana. Maafisa wa usalama nchini Nigeria wamekua wakiimarisha operesheni dhidi ya wapiganaji hao kabla ya siku ya mwisho iliyotolewa na Rais kuangamiza kabisa Boko Haram.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Boko Haram

Nigeria imekua ikikabiliana na maasi ya wapiganaji hao wa kiisilamu kwa miaka sita sasa ambao wanataka kuweka dola la kiisilamu kaskazini mwa nchi.

Wapiganaji hao pia wamevuka mipaka na kutekeleza mashambulio katika nchi jirani.

Maelfu ya raia wameuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kukimbia makaazi yao. Wakimbizi wa ghasia hizo wamekua wakiishi katika mazingira magumu bila mahitaji muhimu ya kimsingi.

Huku haya yakijiri watu saba wameuawa katika shambulio linaloshukiwa kutekelezwa na Boko Haram kaskazini mwa nchi ya Cameroon.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanajeshi wa Nigeria

Maafisa wamesema kulitegwa mabomu mawili lakini ni moja tu lililolipuka. Cameroon ni moja wapo ya mataifa yanayoshirikiana na Nigeria kukabiliana na kundi la Boko Haram.

Mataifa mengine ni Chad, Niger na Benin ambayo yametoa majeshi yao kupambana na wapiganaji hao .