Mkutano Paris kuhitaji siku moja zaidi

Paris Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kuna matumaini tele kwamba kutakuwa na maafikiano

Washiriki katika mkutano mkuu kuhusu mabadiliko ya tabia nchini mjini Paris wamesema watahitaji siku moja zaidi kufanikisha makubaliano, Ufaransa imesema.

“Mambo yanaendelea vyema hata hivyo,” amesema Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius, anayeongoza mkutano huo.

Lakini pande mbalimbali zinahitaji kulegeza zaidi msimamo kabla ya maafikiano, mwandishi wa BBC aliyeko Paris anasema.

Mkataba ambao utatiwa saini Paris utaanza kutekelezwa 2020.

Bw Fabius ameambia runinga ya Ufaransa kwamba “hali ni nzuri, na kuna matumaini” kwamba mkataba mpya utawasilishwa Jumamosi.

Washiriki kwenye mkutano huo wa Umoja wa Mataifa unaoitwa COP21 wamekuwa wakifanyia kazi mswada uliotayarishwa na afisi ya rais wa Ufaransa tangu Jumatano.

Hiyo ilionekana kama hatua kuu baada ya mashauriano yaliyoanza 2011 kutafuta mktaba mpya ulimwenguni wa mkakati wa muda mrefu wa kukabili mabadiliko ya tabia nchi.

Haki miliki ya picha epa
Image caption Ufaransa imefanikiwa kuongoza masuala mengi yaliyokuwa na utata

Afisi ya rais wa Ufaransa inaonekana kutayarisha mswada ambao ulifanikiwa kutatua baadhi ya masuala makuu.

Mataifa yaliyo hatarini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanaonekana kufanikiwa sana katika mazungumzo hayo.

Nyaraka iliyotayarishwa inasema pesa za kusaidia mataifa hayo kupata kawi safi na kukabiliana na mabadiliko hayo zinafaa kutolewa kufikia 2020.