Mataifa 'yakubaliana' kuhusu mkataba Paris

Paris Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mataifa mengi yameridhishwa na mswada uliowasilishwa Paris

Marekani pamoja na kundi la mataifa ya G77 na kundi la Uchina, kwa pamoja wakiwakilisha mataifa 130 yanayoendelea, wote wanaunga mkono mswada wa mkataba mpya wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi uliotolewa baada ya mazungumzo Paris.

Kamishna wa mazingira wa Muungano wa Ulaya Miguel Arias Canete pia amesema muungano huo unaunga mkono mkataba huo ambao umetolewa baada ya karibu wiki mbili za mazungumzo.

Mataifa mengi yanayoendelea yameeleza kuridhishwa na mkataba huo ambao unalenga kuweka kiwango cha ongezeko la joto duniani katika chini ya nyuzi 2 za celsius.

"Tumeungana sote, tuko pamoja. Tuna furaha kwenda nyumbani na mkataba huu," amenukuliwa akisema Nozipho Mxakato-Diseko, kiongozi wa Afrika Kusini katika mazungumzo hayo, ambaye pia ndiye msemaji wa kundi la G77

Mafanikio hayo yalipatikana saa 16 baada ya wakati uliotarajiwa.

Mswada huo tayari umetafsiriwa kwa lugha sita rasmi za Umoja wa Mataifa

Wadadisi wa mambo wanasema bado huo hauwezi kuchukuliwa kama mkataba kamili.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bw Fabius alikuwa ameeleza matumaini mkataba utapatikana

Mswada huo utaidhinishwa iwapo hakutakuwa na pingamizi kwenye mkutano wa mawaziri kutoka nchi mbalimbali, ambao unatarajiwa kufanyika baadaye mjini Paris.

Lakini waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa Bw Laurent Fabius, aliyeongoza mazungumzo hayo, alikuwa awali amesema kwamba “hali ni nzuri zaidi” ya kupatikana kwa mkataba thabiti na wa kufana.