Wataliban walioshambulia Kabul wauawa

Kandahar Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jumanne wiki hii, watu 50 waliuawa Kandahar

Wapiganaji wanne wa kundi la Taliban walioshambulia mgahawa ulio karibu na ubalozi wa Uhispania mjini Kabul wameuawa.

Maafisa wa serikali ya Afghanistan wamesema polisi wanne wa Afghanistan, na walinzi wawili wa Uhispania pia wamefariki katika shambulio hilo.

Ripoti zinasema raia mmoja pia wameuawa kwenye shambulio hilo lililotekelezwa baadaye Ijumaa.

Kundi la Taliban lilisema wapiganaji wake walilipua bomu lililotegwa kwenye gari eneo la Sherpur kabla ya kuingia eneo hilo.

Kundi hilo lilithibitisha vifo vya wapiganaji wake lakini tovuti ya kundi hilo ya Voice of Jihad ilisema waliwaua raia 20 wa Afghanistan na raia kadha wa kigeni.

Kundi hilo limejulikana kwa kutia chumvi idadi ya watu waliouawa kwenye mashambulio .

Ripoti za awali zilikuwa zimedokeza kwamba ubalozi wa Uhispania ulikuwa umeshambuliwa lakini Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy alikanusha hayo.

Shambulio hilo limetekelezwa saa chache baada ya Rais Ashraf Ghani kueleza matumaini ya kurejelewa kwa mazungumzo ya Amani na wapiganaji wa Taliban.

Jumanne, watu 50 waliuawa Taliban waliposhambulia uwanja wa ndege wa Kandahar.