Mvulana akiri mashtaka ya ugaidi Australia

Mvulana Haki miliki ya picha Scott Barbour Getty Images
Image caption Mvulana huyo alikiri kupanga shambulio Mei 8

Mvulana mmoja aliyekamatwa na polisi mjini Melbourne mwezi Mei mwaka huu, amekiri mashtaka yanayohusiana na ugaidi.

Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 17, alikiri kuhusika na kitendo cha kupanga njama ya kutekeleza kitendo cha ugaidi kati ya tarehe 25 Aprili na tarehe 8 Mei mwaka huu.

Alikiri mashtaka hayo kabla ya kesi hiyo kusikilizwa na waendesha mashtaka walifutilia mbali mashtaka mengine mawili yaliyokuwa yakimkabili.

Mahakama hiyo ilifahamishwa kuwa, mvulana huyo alijiandaa kutengeneza vilipuzi baada ya kupata maagizo mtandaoni.

Komputa ya mshukiwa huyo ilikuwa na nyaraka za siri zilizoonyesha jinsi ya kutengeneza mabomu.

Polisi pia walinasa vifaa vya kupikia, mchanganyiko wa unga uliokuwa na makaa ya kutengeneza viberiti na mifereji.

Polisi pia walifahamisha makahama kuwa vitabu vya mafunzo ya itikadi kali vya Kiislamu vilipatikana wakati wa msako huo.

Awali mvulana huyo alifunguliwa mashtaka ya kumiliki vifaa ambavyo vinahusiana na ugaidi na kukataa kutoa kwa polisi nywila yaani neon la siri la kufungua komputa, lakini waendesha mashtaka walitupilia mbali mashtaka hayo.

Mvulana huyo hakuomba kuachiliwa kwa dhamana na sasa angali rumande na anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Alhamisi.