‘Viongozi wa mapinduzi’ Burundi washtakiwa

Burundi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu zaidi ya 240 wameuawa Burundi tangu mwezi Aprili

Waziri wa zamani wa ulinzi nchini Burundi Cyrille Ndayirukiye amefikishwa kortini akishtakiwa kupanga mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.

Bw Ndayirukiye amefikishwa mbele ya Mahakama ya Juu, pamoja na majenerali 27 wa jeshi na maafisa wa polisi.

Wanadaiwa kupanga jaribio lililofeli la kupindua serikali ya Rais Pierre Nkurunziza mwezi Mei, upinzani dhidi ya hatua ya Bw Nkurunziza ya kuwania kwa muhula wa tatu ulipokuwa ukiongezeka.

Bw Ndayirukiye na washtakiwa wenzake wamemwambia jaji kwamba wamekuwa wakifungiwa katika “hali ya kinyama”, na wanalazimika kwenda haja kwenye ndoo.

Image caption Jenerali Ndayirukire na wenzake wamekataa kujibu mashtaka

Wamesema hawatajibu mashtaka hadi hali gerezani iimarishwe.

Washtakiwa hao 28 wanadaiwa pia kuchochea mauaji na uharibifu wa mali.