Mashabiki wasubiri filamu mpya ya Star Wars

Filamu Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mashabiki wamekuwa wakisubiri nje ya kumbi tatu za sinema Los Angeles

Filamu ya karibuni zaidi ya mwendelezo wa filamu za Star Wars, The Force Awakens, itaonyeshwa kwa mara ya kwanza katika mji wa Los Angeles.

Filamu hiyo, ya saba katika mwendelezo wa filamu hizo, imewaleta pamoja waigizaji wa kwanza kabisa Harrison Ford, Mark Hamill na Carrie Fisher.

Waigizaji Waingereza John Boyega, Daisy Ridley na Gwendoline Christie wote wanatarajiwa kuhudhuria hafla ya kuzindua filamu hiyo katika eneo la Hollywood Boulevard.

Mashabiki wamekusanyika nje ya kumbi tatu za sinema tangu wiki jana.

Filamu hiyo itaonyeshwa katika kumbi tatu - TCL Chinese Theatre, Ukumbi wa Dolby – ngome ya Oscars – na Ukumbi wa El Capitan.

Ukumbi wa TCL Chinese Theatre, awali ukifahamika kama Grauman's Chinese Theatre, ndio ulioonyesha filamu ya kwanza kabisa ya Star Wars mwaka 1977.

Mashabiki waliambiwa lazima wawe wamekaa kwenye foleni zaidi ya saa 24 ndipo waruhusiwe kununua mbili. Aliyekaa saa 24 zaidi ya saa 48 ataruhusiwa kununua tiketi nyingine.

Filamu hiyo ya The Force Awakens itaonyeshwa mara ya kwanza Uingereza mjini London Jumatano.